Jeshi la Guinea-Bissau ladai limechukua udhibiti wa nchi (6)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 27, 2025
Jeshi la Guinea-Bissau ladai limechukua udhibiti wa nchi
Picha iliyopigwa Novemba 26, 2025 ikionyesha mwonekano wa mji mjini Bissau, Guinea-Bissau. (Xinhua/Darcio)

BISSAU - Vikosi vya Jeshi la Guinea-Bissau vimetangaza jana Jumatano kupitia televisheni ya taifa kwamba vimechukua rasmi mamlaka zote za nchi hiyo na kuweka hatua kadhaa za dharura ambapo jeshi, lililopewa jina la "Kamandi Kuu ya Kijeshi ya Kurejesha Usalama wa Taifa na Utaratibu wa Umma," limesema hatua hiyo imekusudiwa kukabiliana na vitendo vya wanasiasa fulani wanaojaribu kuvuruga nchi.

Msemaji wa jeshi hilo Dinis N'Tchama amesema kupitia televisheni kwamba jeshi hilo limechukua udhibiti wa Guinea-Bissau, huku mchakato unaoendelea wa uchaguzi umesimamishwa mara moja.

Amesema, hatua nyingine ni pamoja na kufungwa kwa taasisi za umma, kusimamishwa kwa shughuli za vyombo vya habari, vilevile kufungwa kwa mipaka yote ya nchi kavu, baharini, na anga. Amesema, jeshi limetoa amri ya marufuku ya kutoka nje ya lazima kuanzia saa 1:00 jioni hadi saa 12:00 asubuhi kwa saa za Guinea-Bissau.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, majira ya saa 7:00 mchana, milio mizito ya risasi ilisikika karibu na ikulu ya rais katikati mwa Mji wa Bissau, mji mkuu wa nchi hiyo. Wakazi wa karibu walikimbia, na wanajeshi baadaye walichukua udhibiti wa barabara kuu inayoelekea ikulu.

Mwandishi wa habari wa Xinhua ameshuhudia kwenye eneo la tukio kwamba hadi kufikia wakati wa kuripoti habari hii, mji wa Bissau ulikuwa umerejea katika utulivu. Amesema, huku muda wa amri ya kutotoka nje ukiwa umekaribia, idadi ya watembeaji kwa miguu na magari barabarani ilikuwa imepungua kwa kiasi kikubwa, lakini idadi kubwa ya wanajeshi bado walikuwa wakionekana kwenye maeneo ya kimkakati katika sehemu mbalimbali ya mjini.

Ubalozi wa China nchini Guinea-Bissau umetoa tahadhari ya dharura siku hiyo hiyo, ukiwahimiza raia wa China nchini humo kuimarisha hatua za usalama.

Guinea-Bissau siku ya Jumapili ilianza uchaguzi wake wa rais na wabunge, huku wapiga kura zaidi ya 960,000 waliojiandikisha wakiwa walijiandaa kuchagua mkuu mpya wa nchi na wabunge 102 wa Bunge la Taifa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha