Moto wadhibitiwa katika sehemu ya makazi ya Hong Kong, msaada watolewa kwa wakazi (3)

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 28, 2025
Moto wadhibitiwa katika sehemu ya makazi ya Hong Kong, msaada watolewa kwa wakazi
Waokoaji wakimhamisha mtu aliyejeruhiwa kwenye eneo la ajali ya moto ya sehemu ya makazi huko Hong Kong, kusini mwa China, Novemba 27, 2025. (Xinhua/Chen Duo)

HONG KONG – Askari wa Zimamoto wanafanya kazi kukimbizana na muda ili kuzima moto mkubwa ambao umeharibu sehemu ya makazi huko Hong Kong tangu juzi Jumatano alasiri, huku msaada na uungaji mkono ukitolewa kutoka jamii mbalimbali kote Hong Kong na kwingineko.

Hadi kufikia leo Ijumaa mchana, moto huo uliozuka kwenye Makazi ya Wang Fuk ulikuwa umesababisha vifo vya watu 128 na kujeruhi watu 76, kwa mujibu wa Idara ya Zima Moto (FSD) ya Hong Kong. Idara hiyo imesema, Askari wa zimamoto kumi na mmoja wamejeruhiwa, na mmoja amefariki wakati wa kazi ya uokoaji.

Askari wa zimamoto wamemwokoa mtu mmoja kutoka eneo lililoathiriwa majira ya karibu saa 12:45 jioni jana Alhamisi, FSD imesema. Kwenye mkutano na waandishi wa habari wa awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mkoa wa Utawala Maalum wa Hong Kong (HKSAR) John Lee alisema watu 55 wameokolewa kutoka kwenye majengo hayo.

Lee ameongeza kuwa serikali ya HKSAR inatoa ruzuku ya fedha ya dola 10,000 za Hong Kong (dola karibu 1,286 za Marekani) kwa kila kaya iliyoathiriwa na ajali hiyo ya moto jana Alhamisi jioni.

"Serikali ya HKSAR imeanzisha makazi tisa ya dharura ili kuwaweka wakazi. Kwa mipango ya muda mrefu zaidi, serikali ya HKSAR itakusanya rasilimali za umma na binafsi ili kutoa nyumba takriban 1,800 za makazi ya mpito,” Lee amesema.

Makazi ya Wang Fuk, mradi wa majengo mengi ya nyumba za bei nafuu uliokamilishwa mwaka 1983, ulikuwa na wakazi wapatao 4,000 katika nyumba 1,984. Moto huo ulipozuka, majengo yote manane yalikuwa yamefunikwa na wavu wa kijani na jukwaa kutokana na mradi mkubwa wa ukarabati uliokuwa ukiendelea. Moto huo ulianza kutoka kwenye jukwaa nje ya jengo moja na kusambaa hadi kwenye mengine sita.

Watu watatu wanaohusika na ukarabati huo walikamatwa mapema jana Alhamisi kwa tuhuma za mauaji bila kukusudia, huku uchunguzi wa polisi ukibaini nyenzo zinazoweza kuwaka zilizokuwa zimefunika majengo hayo kama sababu inayowezekana ya kusambaa kwa haraka kwa moto huo.

Tume Huru ya Kupambana na Rushwa ya Hong Kong jana Alhamisi ilianzisha uchunguzi kuhusu madai ya ufisadi kwenye mradi huo wa ukarabati.

Serikali ya HKSAR imeamuru ukaguzi wa usalama wa mji mzima kwenye majukwaa na nyenzo zote za ujenzi zinazotumika katika miradi ya ukarabati wa majengo, kwa mujibu wa afisa mtendaji mkuu.

Serikali ya HKSAR jana Alhamisi ilitenga dola milioni 300 za Hong Kong ili kuanzisha mfuko wa kusaidia wakazi wa Makazi ya Wang Fuk kukabiliana na matatizo. Watu binafsi wanaweza kutuma mchango yao kwa aina zote za sarafu kwenye akaunti za benki za mfuko huo.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Deng Jie)

Picha