Maonyesho ya Sanaa yafuatilia mali ya urithi wa TAZARA na urafiki kati ya China na Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 01, 2025
Maonyesho ya Sanaa yafuatilia mali ya urithi wa TAZARA na urafiki kati ya China na Afrika
Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Ashatu Kijaji (wa tatu kushoto), Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian (wa nne kulia), na wageni wengine waalikwa wakipiga picha ya pamoja kwenye hafla ya kufungua maonyesho ya sanaa yenye kichwa cha "Bega kwa Bega kwenye Njia Moja" iliyofanyika Dar es Salaam, Tanzania, Novemba 26, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

DAR ES SALAAM - Maonyesho ya sanaa yenye kichwa cha "Bega kwa Bega kwenye Njia Moja" yamefunguliwa Dar es Salaam, Tanzania, yakiwaalika watazamaji kujionea historia ya zamani na zama za sasa zenye nguvu hai za Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), ambayo ni alama ya kudumu ya urafiki kati ya China na Afrika.

Maonyesho hayo yaliyofunguliwa Jumatano iliyopita, yanaonesha kazi za sanaa 46 -- 11 za wasanii wa Tanzania na 35 za wenzao Wachina – yakileta kumbukumbu za Solomon Mwakasanga mwenye umri wa miaka 73.

Mwakasanga, ambaye alijiunga na TAZARA mwaka 1970 akiwa karani na alistaafu mwaka 2005 akiwa msimamizi mkuu wa stesheni, alisimama kwa muda mrefu mbele ya picha inayoonyesha wafanyakazi wakibeba mataluma ya reli katika ardhi yenye mazingira magumu.

"Tulijenga reli hii pamoja. Ilibadilisha muunganisho wa kikanda, na ilibadilisha maisha yetu. Nimenufaika sana kutokana nayo." amesema.

Maonyesho hayo, yenye kichwa cha "Bega kwa Bega kwenye Njia Moja," yanahusisha nyenzo za kumbukumbu, historia simulizi, na kazi za sanaa za zama za sasa ili kuadhimisha miaka 50 tangu kukamilika kwa Reli ya TAZARA.

Maonyesho hayo yaliyopangwa kuendelea hadi Januari 26, 2026, yanafanyika kutokana na maandalizi ya pamoja ya Ubalozi wa China nchini Tanzania, Jumba la Makumbusho ya Kitaifa la Tanzania, Jumba la Makumbusho ya Kitaifa la China, na Shirika la Uhandisi wa Ujenzi la China.

Mwakasanga amekumbuka urafiki wa karibu kati ya wafanyakazi wa Afrika na Wachina ambao waliishi maisha ya kawaida sana bila mahitaji mengi, kufanya kazi pamoja na kukabiliana na magumu, na kujenga reli hiyo kati ya milima na mabonde.

Miongoni mwa wasanii wa Tanzania walioshiriki kwenye maonesho hayo ni Fred Halla mwenye umri wa miaka 50, ambaye ni mwanzilishi wa Urithi Arts, studio ya ubunifu jijini Dar es Salaam. Halla alikua huku akiangalia treni za TAZARA zikipita mara kwa mara katika maskani aliyozaliwa na kukulia, na kujiunga na maonyesho hayo kumemruhusu asimulie hadithi za reli kwa mtazamo wake wa kisanii.

"Kwangu mimi, TAZARA siyo tu reli, nayo imeonesha ushirikiano kati ya Tanzania, Zambia, na China, na alama ambayo imegusa fursa za uchumi, elimu, afya, na mawasiliano ya kitamaduni." amesema.

Maonyesho hayo yanajitokeza katika sehemu nne za mada, ambazo ni "Matarajio Makuu, Zamani Tukufu," "Kuendelea kufuata nyayo za watangulizi, kufanya kazi kwa kujipatia Matokeo Halisi, kuendeleza Urafiki na Dhamira Njema," "Marafiki Kuvuka Vizazi," "Mazingira kando ya Reli ya Ajabu ya Tanzania-Zambia," na pia "Ukuta wa Sauti."

Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Ashatu Kijaji ameyaelezea maonyesho hayo kuwa ni "darasa hai" ambalo linahifadhi hali ya kujitoa mhanga na mafanikio ya wafanyakazi na wahandisi. Pia amesisitiza umuhimu wa Reli ya TAZARA ikiwa mali yenye thamani ya urithi wa mshikamano kati ya Afrika na China.

Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesisitiza maana muhimu ya kihistoria na umuhimu wake wa alama ya reli hiyo, akiiita "Reli ya Uhuru," kwa kuunga mkono harakati za ukombozi kusini mwa Afrika, na "Reli ya Urafiki," inayowakilisha uhusiano wa kina na wa kudumu kati ya China na Afrika.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha