Lugha Nyingine
Sera ya Russia ya msamaha wa visa kwa raia wa China yaanza kutumika

Picha hii iliyopigwa Desemba 1, 2025 ikionyesha mandhari ya Kremlin mjini Moscow, Russia. (Xinhua/Hao Jianwei)
MOSCOW - Rais wa Russia Vladimir Putin amesaini amri jana Jumatatu inayoruhusu raia wa China kuingia Russia bila visa kufanya utalii au biashara ndani ya muda usiozidi siku 30, kwenye msingi wa kanuni ya kuleta manufaa kwa pande mbili.
Amri hiyo imeanza kutumika mara tu baada ya kusainiwa.
Chini ya amri hiyo, hadi Septemba 14, 2026, raia wa China wenye pasipoti za kawaida za Jamhuri ya Watu wa China wana haki ya kuingia Russia na kukaa kwa muda usiozidi siku 30 kwa kufanya shughuli za kuwatembelea jamaa, kufanya safari za kikazi, utalii, kushiriki katika shughuli zinazohusu sekta za sayansi, utamaduni, jamii, siasa, uchumi au michezo vilevile kusafiri kupitia eneo la Russia kuunganisha ndege na kutoka nje ya nchi, bila kuhitaji kupata visa.
Amri hiyo imesema, hatua hiyo haihusu raia wa China wanaoingia Russia kwa ajili ya kufanya kazi, masomo au kukaa nchini humo, wala haihusu wale wanaofanya usafiri wa barabarani wa kimataifa kama madereva, wafanyakazi wa vyombo vya usafiri, wasafirishaji mizigo au wakalimani wanaoambatana na vyombo kama hivyo vya usafiri.
"Sera ya msamaha wa visa kwa raia wa China inatarajiwa kwamba, idadi ya watalii wanaoingia Russia kutoka China itaongezeka kwa asilimia 30 hadi 40 wakati wa majira ya joto," amesema Alexander Musikhin, naibu mkuu wa utalii wa wageni wanaoingia Russia wa Jumuiya ya Waendeshaji wa Shughuli za Utalii ya Russia.
"Sera hii imekuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu kwa shughuli yetu ya utalii. Watalii wa kujitegemea wanaowasili kutoka China hadi Russia wanaweza kuongezeka kwa mara 1.5 hadi 2, ikiwa ni pamoja na safari za kikazi," amesema Alexander Bragin, mkurugenzi wa Jumuiya ya waendeshaji wa shughuli za Utalii ya Russia.
China ilitangaza Septemba 2 mwaka huu majaribio ya mwaka mmoja ya sera ya siku 30 ya msamaha wa visa kwa raia wa Russia wenye pasipoti za kawaida, ambayo yalianza kutumika Septemba 15. Sera hiyo inahusu raia wa Russia wanaokuja China kwa kufanya biashara, utalii, kutembelea jamaa au marafiki, kushiriki katika shughuli mbalimbali za mawasiliano, au kuingia China kuunganisha ndege kwenda sehemu nyingine.

Picha hii iliyopigwa Desemba 1, 2025 ikionyesha mandhari ya Kremlin mjini Moscow, Russia. (Xinhua/Hao Jianwei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



