Kampuni ya China yafanya kampeni ya kuzuia VVU/UKIMWI nchini Uganda

(CRI Online) Desemba 02, 2025

Huku jana Jumatatu ilikuwa ni Siku ya UKIMWI Duniani, Kundi la Kampuni za Uhandisi wa Reli la China nchini Uganda limefanya kampeni ya kuzuia VVU/UKIMWI miongoni mwa wafanyakazi wake na jamii za wenyeji.

Kampuni hiyo ikishirikiana na Shirika la Uungaji Mkono wa Mapambano Dhidi ya UKIMWI (TASO), ambalo ni shirika lisilo la kiserikali, imetoa huduma ya ushauri nasaha na upimaji wa VVU bila malipo katika ofisi kuu ya kampuni hiyo iliyopo mjini Kampala.

Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Liu Qiang, amesema tukio hilo limefanyika ili kuongeza uelewa wa kuzuia VVU/UKIMWI miongoni mwa wafanyakazi na kujenga kinga kubwa ya ulinzi wa afya.

Liu amesema kampuni hiyo inatilia maanani sana mahitaji ya kiafya ya wafanyakazi wake.

Wakati wa tukio hilo, wafanyakazi walipima kwa hiari VVU/UKIMWI, kupokea vifaa vya kupima kwa njia ya mdomo bila malipo kutoka TASO, na kupata elimu ya afya iliyojikita katika maambukizi, kinga, na matibabu dhidi ya VVU.

Ripoti ya hivi karibuni kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI ya Uganda iliyo chini ya serikali ilionesha kuwa nchi hiyo iko njiani kukomesha hali ya UKIMWI kuwa tishio la afya ya umma ifikapo 2030, kufuatia kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU na vifo vinavyohusiana na UKIMWI.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha