Lugha Nyingine
Mkoa wa Xinjiang wa China wawa mwenyeji wa jukwaa la kikanda ili kuimarisha uhusiano na biashara na Asia ya Kati

Wageni wakihudhuria Jukwaa la Tianshan la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia ya Kati mjini Urumqi, Mkoa Unaojiendesha wa Kabila la Wauygur wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, Desemba 2, 2025. (Xinhua/Zhou Shengbin)
URUMQI - Jukwaa la Tianshan la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia ya Kati limefunguliwa rasmi jana Jumanne mjini Urumqi, Mkoa Unaojiendesha wa Kabila la Wauygur wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, likivutia maofisa wa serikali na wajumbe kutoka mashirika ya mambo ya fedha, jumuiya za washauri bingwa na sekta binafsi zaidi ya 300 kujadili kuhimiza biashara na uwekezaji katika kanda nzima.
Jukwaa hilo la siku mbili, lenye kaulimbiu ya "Kuanzisha Mafungamano ya Mawasiliano na Uwekezaji katika Asia ya Kati," limeshirikisha nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Kikanda ya Asia ya Kati (CAREC) ambapo majadiliano yalilenga biashara, usafiri, nishati na mafungamano ya mawasiliano ya kidijitali katika kanda hiyo.
Waziri wa Fedha wa China Lan Fo'an akitoa hotuba ya kufungua jukwaa alisema kuwa, ushirikiano wa CAREC umepata maendeleo dhahiri na unapaswa kupanuka kwa ukubwa na kina ili kunufaisha watu katika nchi wanachama.
"Jukwaa la Tianshan litatumika kama daraja linalounganisha watunga sera, mashirika binafsi, washirika wa maendeleo na mashirika ya utafiti ili kutoa mipango ya kukabiliana na changamoto zinazotukabili pamoja," amesema Charymuhammet Shallyyev, Mkurugenzi wa Taasisi ya CAREC, ambayo imeandaa shughuli za jukwaa hilo.
Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa kituo chake halisi mjini Urumqi mwaka 2015, taasisi hiyo imefanya utafiti wa miradi zaidi ya 180 na kuwasaidia maofisa wa serikali zaidi ya 2,000 wa nchi wanachama wa CAREC kuongeza uwezo wao katika kazi kwa kupitia miradi 150 ya utoaji mafunzo.
Waziri wa Mipango, Maendeleo na Mambo Maalum wa Serikali Kuu ya Pakistan Ahsan Iqbal amesema kuwa mazingira ya sasa ya kimataifa yanapitia mabadiliko makubwa, huku Asia ya Kati na Asia Kusini zikiibuka kuwa injini kuu zinazohimiza ukuaji wa uchumi wa dunia.
Ametaja miradi iliyofanikiwa kati ya Pakistan na China na akitoa wito wa ushirikiano wa kina zaidi katika viwanda, mawasiliano kati ya watu, na kuanzisha ushirikiano wa kina zaidi katika kilimo na teknolojia.
Jukwaa hilo pia limeshuhudia uzinduzi wa kituo cha utafiti wa ushirikiano wa mambo ya fedha cha Asia ya Kati, kilichoanzishwa na Taasisi ya CAREC na idara ya mambo ya fedha ya kikanda ya Xinjiang.
Asia ya Kati ni kituo muhimu cha kiini cha Eurasia. Biashara kati ya China na Asia ya Kati imeongezeka kwa kasi tangu Mkutano wa kwanza wa viongozi wa China na Asia ya Kati mwezi Mei mwaka 2023, thamani ya jumla ya biashara hiyo ikifikia dola za Kimarekani bilioni 94.8 mwaka 2024. Xinjiang inayopakana na nchi nyingi za Asia ya Kati, inaimarisha kazi yake muhimu ya kuwa kituo kikuu kwenye Ukanda Mmoja, Njia Moja.

Mzia Giorgobiani, Naibu Waziri wa Miundombinu wa Georgia, akizungumza kwenye Jukwaa la Tianshan la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia ya Kati mjini Urumqi, Mkoa Unaojiendesha wa Kabila la Wauygur wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, Desemba 2, 2025. (Xinhua/Zhou Shengbin)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



