Lugha Nyingine
Mapigano yapamba moto mashariki mwa DR Congo huku jeshi na M23 wakilaumiana kwa kukiuka usimamishaji vita
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Kundi la Waasi wa M23 wametupiana lawama za kukiuka makubaliano ya kusimamisha mapigano mashariki mwa nchi hiyo, kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa mashambulizi mapya licha ya upatanishi unaoendelea wa kimataifa.
Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, msemaji wa Jeshi la DRC (FARDC), Sylvain Ekenge, amelaani mashambulizi mfululizo ya M23 kwenye maeneo ya kijeshi katika Jimbo la Kivu Kusini, ambapo maeneo kadhaa, yakiwemo mji mkuu wa jimbo hilo, Bukavu, yako chini ya udhibiti wa waasi.
Waasi wa M23, kwa upande wao, wameishutumu Kinshasa kwa "kuanzisha mashambulizi makubwa katika maeneo yenye watu wengi ikiwemo kwenye safu zote za mstari wa mbele" katika jimbo hilo la Kivu Kusini.
Msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka amedai kwamba vikosi vya FARDC vilishambulia mji wenye watu wengi wa Kamanyola, njia panda ya kimkakati ambayo sasa inashikiliwa na waasi hao, na kuua raia watatu na wengine watano kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya Umoja wa Mataifa, mapigano makali yalitokea mapema jana Jumanne katika pande nyingi za Kivu Kusini, na kuongeza hofu kwa raia walionaswa kati ya pande zinazopigana.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



