Sera ya China ya kutotoza ushuru inafungua mlango mpya kwa mauzo ya nje ya kahawa ya Uganda: mjasiriamali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 03, 2025

KAMPALA - Sera iliyopanuliwa ya China ya kutotoza ushuru bidhaa za Afrika inatarajiwa kuhimiza kwa kiasi kikubwa mauzo ya nje ya kahawa ya Uganda na kuongeza mapato ya familia, Nelson Tugume, afisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Inspire Africa, ambayo inamiliki Eneo Maalum la Kahawa ya Afrika katika wilaya ya Ntungamo, magharibi mwa Uganda ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Amesema kwamba sera hiyo mpya ya China inatoa mazingira mazuri zaidi ya biashara ikilinganishwa na masoko ambayo yanaendelea kutoza ushuru mkubwa kwa bidhaa za Afrika.

Kuanzia Desemba 1, 2024, China ilianza kutoa msamaha wa Ushuru kwa bidhaa zote kutoka nchi zilizoko nyuma kimaendeleo ambazo zina uhusiano nazo wa kidiplomasia, zikiwemo nchi 33 za Afrika.

Upanuzi wa sera hiyo ya kutotoza ushuru ulitangazwa baadaye ili kujumuisha asilimia 100 ya bidhaa kutoka nchi zote 53 za Afrika ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia na China.

Tugume amesema sera hiyo, pamoja na ongezeko la mahitaji ya kahawa ya China na hali ya kutokuwa na uhakika katika nchi zinazozalisha kahawa kwa wingi, hutoa fursa kwa wakati kwa wakulima wa Uganda wanaotafuta masoko mapya na imara.

"Kwa kampuni yoyote inayojitahidi kukua, inaenda mahali ambapo mazingira ni mwafaka," amesema, kabla ya shehena ya kahawa iliyonunuliwa na kusindikwa nchini Uganda kusafirishwa China.

Amesema kwamba ili kufikia viwango vya China na kuhakikisha usambazaji endelevu, Uganda lazima ijiandae vya kutosha.

"Tumeona nchi zikikua na kujifunza kutoka kwa kila mmoja," Tugume amesema, akiongeza kuwa wafanyakazi zaidi ya 40 wa Inspire Africa walikuwa wamerudi hivi karibuni kutoka China baada ya kupata ujuzi wa kiufundi.

Amesema wafanyakazi wengine 40 watakwenda nchini China ili kupata weledi wa teknolojia zinazotumika katika mashine za kusindika kahawa.

"Ili watu wetu waelewe, lazima kuwe na uhamishaji wa maarifa. Tuna washirika nchini China ambao wameturuhusu kuingia kwenye viwanda vyao na kujifunza namna teknolojia hizi zinavyofanya kazi," ameongeza.

Takwimu kutoka Wizara ya Kilimo, ufugaji na Uvuvi ya Uganda zinaonyesha kuwa mauzo ya kahawa kwenda China yaliongezeka kwa asilimia 190 mwezi Machi 2025 pekee, na kuifanya China kuwa soko la pili kwa ukubwa la kahawa la Uganda barani Asia.

Mapema mwezi huu, wizara hiyo pia ilitoa ripoti ikisema kwamba wauzaji nje wa Uganda walipata mikataba yenye thamani ya dola milioni 3 za Marekani kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China.

Kahawa inaendelea kuwa moja ya bidhaa muhimu za Uganda kwa mageuzi ya muundo wa uchumi, huku familia takribani milioni 1.8 zikitegemea zao hilo, kwa mujibu wa wizara hiyo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha