DRC na Rwanda zasaini makubaliano ya amani, zafungua rasilimali muhimu za madini kwa Marekani

(CRI Online) Desemba 05, 2025

WASHINGTON - Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa mwenyeji wa wenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda mjini Washington D.C Marekani jana Alhamisi, akiwashuhudia wakisaini makubaliano ya amani yenye lengo la kumaliza vita vya miongo kadhaa mashariki mwa DRC wakati huohuo wakifungua rasilimali zao muhimu za madini kwa Marekani.

Marais Felix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda wamesaini makubaliano hayo kwenye hafla iliyofanyika katika Taasisi ya Amani ya Marekani, ambayo imepewa jina jipya la "Taasisi ya Amani ya Donald J. Trump" na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani siku moja mapema.

Eneo la Mashariki mwa DRC limekuwa likikumbwa na miongo kadhaa ya migogoro, iliyozidishwa na kuibuka tena kwa waasi wa Harakati ya Machi 23 (M23) tangu mwishoni mwa mwaka 2021. DRC inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi hilo, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha.

Kwenye hafla hiyo, Rais Trump pia alitangaza makubaliano ya pande mbili ya Marekani na nchi hizo mbili za Afrika, ambapo kampuni za Marekani zitapata madini muhimu ya eneo hilo.

"Na tutahusika katika kutuma baadhi ya kampuni zetu kubwa na nzuri za Marekani kwa nchi hizo mbili," Trump amesema.

Mwezi Juni, makubaliano ya awali ya amani yalitiwa saini na mawaziri wa mambo ya nje wa DRC na Rwanda mjini Washington.

Jeshi la DRC na waasi wa M23 siku ya Jumanne walitupiana shutuma za kukiuka makubaliano ya kusimamisha mapigano mashariki mwa nchi hiyo, huku kila upande ukimlaumu mwingine kwa mashambulizi mapya licha ya upatanishi wa kimataifa.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha