Lugha Nyingine
Rais Xi afanya mazungumzo na mwenzake Macron, akitoa wito wa kupanua ushirikiano katika maeneo mbalimbali

Rais Xi Jinping wa China na mkewe Peng Liyuan wakipiga picha na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na mkewe Brigitte Macron kabla ya mazungumzo kati ya viongozi hao wawili mjini Beijing, mji mkuu wa China, Desemba 4, 2025. (Xinhua/Huang Jingwen)
BEIJING - China na Ufaransa zinapaswa kutumia kikamilifu fursa na kupanua ushirikiano, Rais Xi Jinping wa China amesema katika mazungumzo na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye yuko ziarani nchini China yaliyofanyika Beijing jana Alhamisi akiongeza kuwa zikiwa nchi kubwa zinazojitegemea, zenye maono na kuwajibika, China na Ufaransa ni nguvu za kiujenzi katika kusukuma mbele dunia yenye ncha nyingi na kuhimiza mshikamano na ushirikiano miongoni mwa binadamu.
"Kwa sasa, kadri mabadiliko ambayo hayajawahi kuonekana katika miaka 100 iliyopita yanavyoongezeka, binadamu kwa mara nyingine tena anasimama kwenye njia panda, kukabiliwa na machaguo muhimu kuhusu njia yake ya siku za baadaye," Rais Xi amesema, akiongeza kuwa China na Ufaransa zinapaswa kuonyesha uwajibikaji wao, kushikilia mfumo wa pande nyingi, na kusimama kidete kwenye upande sahihi wa historia.
Rais Xi amesema China ina nia ya kushirikiana na Ufaransa ili kila wakati kusonga mbele kutoka maslahi ya msingi ya watu wao na maslahi ya muda mrefu ya jumuiya ya kimataifa, wakati huohuo zikishikilia mazungumzo yenye usawa na ushirikiano wa wazi, ili kuhakikisha kwamba ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Ufaransa unaendelea kusonga mbele kwa kasi tulivu na kustawi katika kipindi cha miaka 60 ijayo, kuonyesha kikamilifu thamani yake ya kimkakati, na kutoa mchango mpya katika kuhimiza dunia yenye ncha nyingi ya usawa na utaratibu vilevile utandawazi wa uchumi duniani wenye manufaa na jumuishi kwa wote.
Rais Xi amesisitiza kwamba bila kujali mazingira ya nje yanayobadilika, China na Ufaransa zinapaswa kuonyesha maono ya kimkakati na hali ya kujitegemea kama nchi kubwa, kuelewana na kuungana mkono katika masuala yanayohusu maslahi ya msingi na mambo makubwa yanayofuatiliwa ya kila upande, na kulinda msingi wa kisiasa wa uhusiano wa pande mbili.
Rais Xi amesisitiza kwamba dunia ya leo haiko katika utulivu, kwani masuala nyeti yenye utata yanaibuka katika sehemu nyingi, akisema kwamba, zikiwa nchi wanachama waanzilishi wa Umoja wa Mataifa na wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, China na Ufaransa zinapaswa kutekeleza ushirikiano wa kweli wa pande nyingi, na kulinda mfumo wa kimataifa unatilia maanani Umoja wa Mataifa na utaratibu wa kimataifa juu ya msingi wa sheria ya kimataifa.
Kwa upande wake Rais Macron amesema kuwa China na Ufaransa zimedumisha mawasiliano ya karibu ya ngazi ya juu, na zimekuwa wakati wote zikiaminiana na kuheshimiana.
"Ufaransa inathamini uhusiano wake na China, inashikilia bila kuyumbayumba sera ya kuwepo kwa China moja, na ina nia ya kuendelea kuzidisha ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya Ufaransa na China," Macron amesema.
Amesema Ufaransa inakaribisha uwekezaji zaidi wa China nchini Ufaransa na itatoa mazingira ya biashara ya haki na yasiyo ya kubagua.
"Kutokana na hali ya kukosekana utulivu kwenye siasa za kijiografia duniani na changamoto kwenye utaratibu wa pande nyingi, ushirikiano kati ya Ufaransa na China ni muhimu zaidi na usiokosekana," Rais Macron amesema, akiongeza kuwa Ufaransa inakubaliana kikamilifu na maoni ya Rais Xi juu ya kuufanyia mageuzi na kuuboresha usimamizi duniani na kuhimiza uchumi wa dunia wenye uwiano zaidi.

Rais Xi Jinping wa China akifanya mazungumzo na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye yuko ziarani nchini China, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Desemba 4, 2025. (Xinhua/Yin Bogu)

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa pamoja wakikutana na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao mjini Beijing, mji mkuu wa China, Desemba 4, 2025. (Xinhua/Yan Yan)

Rais Xi Jinping wa China akifanya hafla ya kumkaribisha Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwenye Ukumbi wa Kaskazini wa Jumba la Mikutano ya Umma kabla ya mazungumzo yao mjini Beijing, mji mkuu wa China, Desemba 4, 2025. (Xinhua/Xie Huanchi)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



