Jeshi la Benin limevunja jaribio la uasi, asema waziri wa mambo ya ndani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 08, 2025

COTONOU - Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Umma wa Benin Alassane Seidou amesema jana Jumapili katika taarifa kwamba, Jeshi la Benin limevunja jaribio la uasi lililolenga kuvuruga nchi na taasisi zake. Hii ilifuatia kundi la wanajeshi kutangaza mapema siku hiyo kupitia kituo cha televisheni cha taifa cha Benin kwamba Rais Patrice Talon "ameondolewa madarakani."

Kwa mujibu wa waziri huyo, vikosi vya jeshi na kamandi zao, "vyenye uaminifu kwa kiapo chao," viliitikia kwa njia ya kijamhuri na viliweza kudhibiti hali, vikizuia jaribio hilo. Serikali imetoa wito kwa umma kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Akizungumza kwa wakati tofauti na jarida la kila wiki la Ufaransa la Jeune Afrique Jumapili asubuhi, Romuald Wadagni, waziri wa serikali anayeshughulikia mambo ya uchumi na fedha, alisema hali "imedhibitiwa."

"Waasi wamenaswa. Tunaendelea kusafisha eneo, lakini bado haijaisha. Tuko salama." Alisema, akiongeza kuwa helikopta zilikuwa zikizunguka kufanya doria kwenye mji na kwamba katikati mwa Cotonou kulilindwa vikali na vikosi vya jeshi.

Wakazi wa eneo hilo wameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwa simu kwamba mjini Cotonou, mji mkuu wa kiuchumi na mji mkubwa zaidi wa nchi hiyo, na maeneo ya jirani, wanajeshi wenye silaha walikuwa wametumwa hasa katika makutano muhimu, huku wakazi wakiendelea na shughuli zao za kila siku na masoko makubwa yakiendelea kuwa wazi.

Mapema Jumapili, kundi la wanajeshi, waliojitambulisha kwa jina la "Kamati ya Kijeshi kwa ajili ya Kujenga Upya (CMR)," walikutana na kuamua kwamba "Bw. Patrice Talon amefukuzwa kazi ya kuwa rais wa jamhuri."

Milio ya risasi iliripotiwa kwenye Kambi ya Guezo, karibu na makazi ya rais mjini Cotonou, na vyombo vya habari nchini humo vilisema wanajeshi walikuwa wamechukua udhibiti wa kituo cha utangazaji cha taifa. Hata hivyo, Ikulu ilisema rais yuko salama na kwamba vikosi vya jeshi la serikali vimerejesha udhibiti wa hali.

Benin, iliyoko Afrika Magharibi, ina eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba takriban 112,000 na idadi ya watu takriban milioni 14.

Kihistoria ikichukuliwa kuwa moja ya nchi zenye amani na utulivu zaidi katika eneo hilo, Benin hata hivyo imepitia mapinduzi na majaribio kadhaa ya mapinduzi baada ya kujipatia uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960.

Utulivu wa kisiasa umekuwa ukidumishwa kwa kiasi kikubwa tangu mwaka 1991, baada ya utawala wa miongo miwili wa Mathieu Kerekou, ambaye aliwahi kubadilisha jina la nchi hiyo kuwa Jamhuri ya Watu wa Benin.

Rais Talon aliingia madarakani kwa mara ya kwanza Machi 2016 na kuchaguliwa tena Aprili 2021. Alikuwa amepangwa kuondoka madarakani baada ya uchaguzi wa rais mwezi Aprili 2026. Wadagni amekuwa akichukuliwa sana kuwa mgombea mwenye nafasi kubwa, huku mgombea wa upinzani Renaud Agbodjo akiwa amezuiliwa na tume ya uchaguzi kutokana na udhamini usiotosheleza.

Mwezi Novemba, bunge la taifa liliidhinisha kuongezwa kwa muhula wa urais kutoka miaka mitano hadi saba, wakati huohuo likiendelea kubakisha kikomo cha mihula miwili.

Matukio ya sasa nchini Benin yanakuja wakati ambapo kuna wimbi jipya la mapinduzi ya kijeshi Afrika Magharibi. Mwishoni mwa Novemba, mapinduzi nchini Guinea-Bissau yalimwondoa madarakani Rais Umaro Embalo kufuatia uchaguzi wenye utata ambapo rais aliye madarakani na upinzani wote walijitangaza washindi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha