Waasi wa M23 wasonga mbele mashariki mwa DRC licha ya makubaliano mapya ya amani yaliyosainiwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 08, 2025

GOMA - Waasi wa Vuguvugu la Machi 23 (M23) wamepanua operesheni zao za kijeshi katika maeneo kadhaa ya Jimbo la Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika siku zilizopita, hata wakati huu ambapo DRC na Rwanda zimesaini makubaliano ya amani mjini Washington, Marekani yanayosifiwa kuwa hatua kubwa kwa kupunguza mivutano katika eneo hilo.

Mapigano yaliongezeka kuanzia Jumanne hadi Ijumaa karibu na Kaziba, Lubarika, Rurambo, Luvungi, na vilele vya Mlima Munanira katika Jimbo la Kivu Kusini. Katika eneo hilo, vikosi vya Burundi na vikundi kadhaa vya wenyeji vimekuwa vikifanya operesheni zao kwa kushirikiana na Vikosi vya Jeshi la DRC (FARDC).

"Waasi wawameanzisha mashambulizi kadhaa dhidi ya maeneo yetu na kujaribu kupita mipango yetu ya ulinzi kwenye mhimili wa Kaziba-Luvungi, lakini jeshi linaendelea kuyazuia majaribio hayo. Mapigano bado yanaendelea," msemaji wa FARDC katika Jimbo la Kivu Kusini, Reagen Mbuyi alisema Alhamisi.

Vyanzo vya habari katika eneo hilo siku ya Ijumaa vilithibitisha kuwa waasi walikuwa wakisonga mbele kuelekea Uwanda wa Ruzizi na ushoroba unaoelekea Uvira kutoka Luvungi – hatua ambayo wachambuzi kadhaa wanaielezea kuwa ni "mabadiliko makubwa ya mstari wa mbele kuelekea Uvira", mji mkuu wa muda wa kiutawala wa Kivu Kusini, baada ya mji mkuu wa jimbo, Bukavu, kutekwa na waasi mwezi Februari.

Wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa wameripoti FARDC imejiondoa katika baadhi ya maeneo, na raia wako wakikimbia maeneo mapya ya mapigano. Wameeleza kuwa, mamia ya familia zimewasili Uvira, wakati huohuo wengine kutoka Kamanyola, eneo muhimu la kimkakati katika jimbo hilo, wamevuka mpaka kuingia Rwanda ili kuepuka mashambulizi.

Uvira iko kwenye barabara muhimu inayounganisha Bukavu na Burundi pamoja na Tanzania na hutumika kama kituo cha huduma cha FARDC katika Uwanda wa Ruzizi, eneo ambalo ni linahifadhi makundi kadhaa ya waasi wa ndani na wa kigeni. Uwezekano wa waasi wa M23 kusonga mbele kuelekea Uvira umeibuka kuwa suala linaloongezeka kuwatia wasiwasi viongozi wa DRC na wadau wa kikanda.

"Kama waasi watafika mitaa ya Uvira, athari za usalama zitakuwa kubwa... Kivu Kusini itakuwa kituo cha pili cha mgogoro" ameonya mchambuzi mmoja wa DRC anayeishi Goma ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Licha ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani yaliyopatanishwa na Marekani kati ya DRC na Rwanda mjini Washington siku ya Alhamisi, kusonga mbele kwa waasi kuliendelea hadi mapema Jumamosi. Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya DRC, Tina Salama, makubaliano hayo yanathibitisha malengo matatu muhimu: kukomesha vurugu mashariki mwa DRC, kurejesha mamlaka na ukamilifu wa ardhi wa DRC, na kuvunja minyororo haramu ya usambazaji wa madini ambayo inafadhili vita.

Eneo hilo la Mashariki mwa DRC kwa muda mrefu limekuwa ikikabiliwa na vurugu mara kwa mara, zikizidishwa na mashambulizi ya Kundi la M23, ambalo Kinshasa inaishutumu Kigali kwa kuliunga mkono. Rwanda inakanusha madai hayo na kuishutumu DRC kwa kushirikiana na Jeshi la Rwanda FDLR, linalohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 2.4 wamekimbia makazi yao tangu Januari 2025, na kufanya idadi ya watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi hiyo hadi karibu milioni 6. Wakongo takriban milioni 1 wamekimbilia nchi jirani, huku watu milioni 27 wakikabiliwa na njaa. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha