Biashara ya nje ya China yadumisha uhimilivu na ukuaji thabiti katika kipindi cha Januari hadi Novemba

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 09, 2025

BEIJING - Biashara ya bidhaa ya China katika miezi 11 ya kwanza ya 2025 imeendelea kuwa thabiti na kukua kwa utulivu licha ya changamoto za nje, takwimu rasmi zilizotolewa na Mamlaka Kuu ya Forodha ya China (GAC) jumatatu zimeonyesha, ambapo jumla ya biashara ya uagizaji na uuzaji wa bidhaa ya China kwa thamani ya yuan iliongezeka hadi kufikia yuan trilioni 41.21 (dola za Marekani karibu trilioni 5.82) katika miezi hiyo 11, ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.6 ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huo.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kiwango hicho cha ukuaji kilibaki sawa ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 3.6 lililorekodiwa katika miezi 10 ya kwanza ya mwaka huu.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa, uuzaji nje yaliongoza upanuzi wa jumla wakati wa kipindi hicho cha Januari hadi Novemba, yakiongezeka kwa asilimia 6.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, wakati huohuo uagizaji bidhaa kutoka nje uliongezeka kwa asilimia 0.2.

Katika miezi 11 hiyo ya kwanza, ASEAN iliendelea kuwa mshirika mkubwa wa biashara wa China, huku jumla ya biashara ya pande mbili ikiongezeka kwa asilimia 8.5 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana hadi kufikia yuan trilioni 6.82, ikichukua asilimia 16.6 ya jumla ya biashara yote ya nje ya China. Ilifuatiwa na Umoja wa Ulaya, kwa biashara ya pande mbili kuongezeka kwa asilimia 5.4 ikilinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana hadi kufikia yuan trilioni 5.37.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa, biashara ya China na Marekani, mshirika wake wa tatu kwa ukubwa wa biashara, ilishuka kwa asilimia 16.9 katika miezi hiyo 11 ya kwanza hadi kufikia yuan trilioni 3.69.

Biashara na nchi za Ukanda Mmoja, Njia Moja iliongezeka kwa asilimia 6 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana hadi kufikia yuan trilioni 21.33, ikichangia asilimia 51.8 ya jumla ya biashara yote ya nje ya China, takwimu hizo zinaonesha.

Takwimu zinaonesha kuwa, kampuni binafsi zilionyesha uhai mkubwa za kuwa kichocheo kikuu cha biashara ya nje ya China, huku thamani za biashara zao za uagizaji na uuzaji nje wa bidhaa zikiongezeka kwa asilimia 7.1 hadi kufikia yuan trilioni 23.52, ikiwa ni asilimia 57.1 ya jumla yote ya taifa.

Biashara ya nje ya China iliendelea kubadilika kimuundo katika miezi hiyo 11 ya kwanza huku uuzaji nje wa bidhaa za mitambo na umeme yakiongezeka kwa asilimia 8.8, na kuchukua asilimia 60.9 ya jumla ya mauzo yote ya nje, ikichochewa na ukuaji mkubwa wa saketi jumuishi na magari.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa, mwezi wa Novemba pekee, biashara ya uagizaji na uuzaji nje bidhaa ya China iliongezeka kwa asilimia 4.1 ikilinganisha na kipindi kama hicho mwaka jana hadi kufikia yuan trilioni 3.9. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha