Lugha Nyingine
UNCTAD yasema thamani ya biashara duniani itazidi dola trilioni 35 mwaka huu
Ripoti mpya iliyotolewa jana Jumanne na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) inaonyesha kwamba, thamani ya biashara duniani katika bidhaa na huduma inatarajiwa kuzidi dola trilioni 35 katika mwaka huu kwa mara ya kwanza.
Ripoti hiyo imesema licha ya mivutano ya siasa za kijiografia, gharama kubwa, na mahitaji yasiyo sawa duniani, ambayo yalipunguza kasi ya ukuaji, biashara duniani iliendelea kukua katika kipindi chote cha nusu ya pili ya 2025.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, biashara duniani inatarajiwa kukua kwa asilimia 7 na kuongeza dola za Marekani trilioni 2.2 kwenye thamani ya jumla ya mwaka jana.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa Asia Mashariki imerekodi ukuaji mkubwa zaidi wa asilimia 9 kwenye mauzo ya nje katika mwaka uliopita, huku biashara ya ndani ya kikanda ikikua kwa asilimia 10. Aidha, biashara ya Afrika na Kusini-Kusini ilirekodi ukuaji mzuri, ikionyesha umuhimu unaozidi kuongezeka wa nchi zenye uchumi unaoibukia katika uchumi duniani.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa, miongoni mwa nchi mbalimbali, China na Korea Kusini zilifanya vizuri zaidi katika Asia Mashariki, huku Brazil na Afrika Kusini zikiwa injini kuu za ukuaji katika Amerika Kusini na Afrika.
Wakati huo huo, ukuaji mkubwa wa mauzo ya nje ya huduma nchini India na China umeonesha jukumu muhimu zaidi la nchi zinazoibuka katika biashara ya kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



