Lugha Nyingine
Rais wa Ghana ahimiza sekta binafsi kuwekeza pamoja kwenye maendeleo ya viwanda vya mambo ya afya barani Afrika

Rais wa Ghana John Dramani Mahama akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Viongozi wa Afrika wa Maonyesho ya Mambo ya Afya Duniani mjini Accra, Ghana, Desemba 9, 2025. (Picha na Seth/Xinhua)
ACCRA - Rais wa Ghana John Dramani Mahama amehimiza wadau wa sekta binafsi kushirikiana na serikali za Afrika katika kuwekeza kwa pamoja kwenye maendeleo ya viwanda vya mambo ya afya ya bara hilo ili kuboresha huduma za afya na utoaji wa huduma.
Kwenye ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa Viongozi wa Afrika wa Maonyesho ya Afya Duniani huko Accra, Ghana, Rais Mahama amesema kwamba Afrika inatafuta mfumo mpya wa ushirikiano, ambao sifa yake siyo ya kutegemea, bali ni kwa kufanya uwekezaji wa pamoja, uvumbuzi, na kunufaika na maadili ya pamoja.
"Kwa hivyo tunatoa wito kwa wafanyabiashara wa utengenezaji wa chanjo kushirikiana nasi kujenga vituo vya uzalishaji wa chanjo barani Afrika. Tunatoa wito kwa kampuni za dawa kupanua wigo katika utengenezaji wa dawa za kiviumbe, bidhaa za dawa, na dawa muhimu za kimsingi barani Afrika," Mahama amesema.
Pia amehimiza kampuni za uvumbuzi wa uthibitishaji wa magonjwa, kampuni za bioteknolojia, na wafanyabiashara wa uzalishaji wa zana na vifaa vya matibabu kuanzisha viwanda vya kuunganisha sehemu pamoja na vituo vya utafiti na maendeleo na viwanda vya kutengeneza bidhaa barani Afrika ili kuhakikisha ufikiaji rahisi kwa taasisi za afya za Afrika.
Rais Mahama amesema bara la Afrika limepata mafunzo muhimu kutokana na janga la COVID-19, wakati bara hilo mara nyingi lilikuwa la mwisho kupokea uungaji mkono wakati wa dharura za afya duniani, na hali hii imeonesha zaidi hitaji la kubadilisha mfumo husika.
Akisisitiza Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika likiwa soko la pamoja kwa watu wapatao bilioni 1.3, limekuwa na mfumo wa ikolojia ya uvumbuzi unaokua na taasisi za usimamizi wa dawa za Afrika zinafanya kazi zao katika kuimarisha kanuni sawa na uwiano wa udhibiti.
Ameeleza imani yake katika mawazo na werevu wa wavumbuzi vijana wa Afrika, wabunifu wa teknolojia ya AI, wavumbuzi wa teknolojia ya matibabu, na wajasiriamali wa mambo ya afya ya kidijitali ili kuanzisha mustakabali wa huduma ya afya wa Afrika na kujenga utaratibu mpya wa afya.
Mkutano huo unahudhuriwa na maofisa wa afya kutoka nchi mbalimbali za Afrika, vilevile wajumbe kutoka Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa na mashirika washirika.

Mwonyeshaji bidhaa akitazama mashine ya kufuatilia wagonjwa kwenye Mkutano wa Viongozi wa Afrika wa Maonyesho ya Afya Duniani mjini Accra, Ghana, Desemba 9, 2025. (Picha na Seth/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



