Kundi la waasi la M23 nchini DRC lasisitiza suluhisho ya kisiasa huku mapigano na vikosi vya serikali yakiendelea

(CRI Online) Desemba 10, 2025

Kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) la nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limesisitiza kupendelea zaidi suluhisho ya kisiasa wakati huu ambapo mapigano yake na vikosi vya Jeshi la DRC yakisonga mbele kuelekea Mji wa Uvira katika Jimbo la Kivu Kusini.

Kiongozi wa kundi la Muungano wa Mto Kongo (AFC), ambalo ni mshirika wa M23, Corneille Nangaa kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, amesema kuwa vuguvugu hilo muda wote limekuwa likitetea suluhisho ya kisiasa.

“Kwa kushiriki au kutoshiriki kwa Rais wa DRC Felix Tshisekedi AFC/M23 zitafanya kazi kutafuta suluhisho za kina za vyanzo vikuu vya mgogoro” amesema, huku akilishutumu jeshi la serikali kwa kuvunja mara nyingi makubaliano ya kusimamisha mapigano.

Katika hotuba yake aliyoitoa Jumatatu wiki hii jijini Kinshasa, Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi alisema, hivi karibuni, kundi la M23 lilifanya shambulizi dhidi ya jeshi la serikali katika Jimbo la Kivu Kusini. Jana Jumanne, vyombo vya habari vya DRC vimeripoti kuwa, mapigano yamefika karibu na mji wa kimkakati wa jimbo hilo, Uvira.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha