Burundi yazindua mpango wa dharura kushughulikia wimbi la wakimbizi kutoka DRC

(CRI Online) Desemba 19, 2025

Serikali ya Burundi imezindua mpango wa dharura wa kusaidia Wakongo elfu 70 ambao hivi karibuni walikimbia vurugu kwenye eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hasa kufuatia mapigano huko Uvira.

Taarifa hiyo imetolewa na Jumatano wiki hii na Waziri wa Mambo ya Ndani, Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Umma wa Burundi Bw. Leonidas Ndaruzaniye baada ya mkutano wa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Mafungamano ya Kikanda na Ushirikiano wa Maendeleo wa Burundi Edouard Bizimana, wanadiplomasia na washirika wa maendeleo.

“Serikali ya Burundi inahitaji angalau dola za kimarekani milioni 33 kuunga mkono watafuta hifadhi 76,015 wa DRC waliopokelewa Burundi tangu tarehe 5 Desemba, kutokana na vurugu zinazoendelea mashariki mwa DRC” amesema.

Ametoa rasmi wito wa dharura kutoka serikali ya Burundi kwa ajili ya mshikamano wa kitaifa na kimataifa ili kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kukabiliana na msukosuko huo wa kibinadamu.

Kwa mujibu wa waziri huyo, katika kipindi cha tarehe 5 hadi tarehe 16 Desemba, Burundi ilisajili wakimbizi 76,015, lakini ni wakimbizi 12,786 tu wamehamishiwa kwenye kambi ya Busuma katika Wilaya ya Ruyigi jimboni Buhumuza.

Amesema, wimbi hilo kubwa la wakimbizi limeleta shinikizo kwa miundombinu iliyopo nchini humo.

(Wahariri wa tovuti:Renato Lu)

Picha