Lugha Nyingine
Rais wa Ghana aapa kuunga mkono ujenzi wa baada ya kimbunga wa Jamaica

Picha iliyopigwa Desemba 17, 2025 ikionyesha gari likisafirisha baadhi ya vifaa vya kusaidia ukarabati wa Jamaica baada ya kimbunga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kotoka mjini Accra, Ghana. (Str/Xinhua)
ACCRA - Rais John Dramani Mahama wa Ghana ameahidi kuwa Ghana inapenda kuunga mkono juhudi za kufufua na kukarabati nchi ya Jamaica kufuatia uharibifu mkubwa uliosababishwa na Kimbunga Melissa.
“Hatua hii kutoka Ghana imechukuliwa kwa kuzingatia uhusiano wa kihistoria ndani ya familia ya Waafrika na Wakaribiani, pamoja na katika moyo wa ushirikiano wa Kusini-Kusini,” Rais Mahama amesema kwenye hafla iliyofanyika Jumatano ya kutumwa kikosi cha wahandisi wa kijeshi wa Ghana kwenda nchi hiyo ya Karibiani kuunga mkono juhudi zinazoendelea za ukarabati na misaada.
Amesema kuwa Ghana imeshatoa cedi milioni 10 za Ghana (takriban dola za Marekani 869,500) kama msaada wa kibinadamu kwa Jamaica, Cuba, na Sudan.
Rais Mahama amesema kwamba uungaji mkono huo wa Ghana kwa juhudi za ukarabati unatokana moja kwa moja na ombi alilotoa binafsi Waziri Mkuu wa Jamaica Andrew Holness.
"Vikosi vyetu vitaenda kusaidia katika ukarabati, ujenzi wa majengo, na pia kutoa msaada kwa watu wa Jamaica," ameongeza.
Rais Mahama amehimiza askari hao kuonyesha tabia nzuri za kupigiwa mfano katika kipindi chote cha utekelezaji wa majukumu yao nchini humo ili kuakisi maadili ya nidhamu na ubinadamu wa askari wa Ghana na kujionesha kama mabalozi wanaostahili wa Jamhuri ya Ghana.
Kikosi hicho cha watu 54, wakiwemo maafisa tisa, kiliondoka Ghana Jumatano kuelekea Jamaica baada ya gwaride fupi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kotoka.

Rais wa Ghana John Dramani Mahama (kulia, mbele) akitoa hotuba kwenye hafla ya kutuma kikosi cha askari wa Ghana kwenda Jamaica kuunga mkono kazi za ukarabati na misaada kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kotoka mjini Accra, Ghana, Desemba 17, 2025. (Str/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



