Lugha Nyingine
Marekani yaongeza operesheni za vizuizi huku meli ya tatu ya mafuta ikizuiliwa karibu na Venezuela
Vyombo vya habari vya Marekani, vikinukuu vyanzo vya serikalini vyenye uelewa wa hali, vimeripoti jana Jumapili kwamba Marekani imeongeza kasi ya operesheni za kuizingira Venezuela kwa kuzuia meli ya tatu ya mafuta kwenye maji ya kimataifa karibu na nchi hiyo katika kipindi cha chini ya wiki mbili.
Shirika la habari la Bloomberg jana Jumapili kwa kunukuu vyanzo vyenye uelewa limeripoti kwamba meli hiyo yenye jina la "Bella 1" ambayo inapeperusha bendera ya Panama na iko chini ya vikwazo vya Marekani, ilipandwa na vikosi vya Marekani wakati ikiwa njiani kuelekea Venezuela kupakia mizigo.
Siku moja mapema, walinzi wa pwani wa Marekani walipanda meli ya mafuta iitwayo "The Centuries", meli ya mafuta yenye kupeperusha bendera ya Panama, ambayo haiko kwenye orodha ya vikwazo vya Marekani.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Anna Kelly alisema kupitia ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba mafuta ghafi yaliyokuwa ndani ya meli hiyo yalitoka kwenye kampuni ya mafuta ya taifa ya Venezuela, ambayo iko chini ya vikwazo vya Marekani.
Tarehe 10 Desemba, vikosi vya Marekani viliikamata meli ya mafuta "Skipper" karibu na maji ya Venezuela, na kutangaza mipango ya Marekani kuchukua mafuta yote iliyokuwa imebeba.
Tarehe 16 Desemba, Rais Donald Trump wa Marekani alitoa amri ya "kuzuiwa kabisa" kwa meli zote za mafuta zilizowekewa vikwazo na Marekani zinazoingia au kutoka Venezuela, na kuitangaza serikali ya sasa ya Venezuela inayoongozwa na Rais Nicolás Maduro kuwa ni "shirika la kigaidi la nje".
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



