China yahimiza kupinga vikali kauli za afisa wa Japan kuhusu kumiliki silaha za nyuklia

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 23, 2025

BEIJING - China imeshtushwa na kauli ya afisa mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Japan aliyesema wazi kwamba Japan inapaswa kumiliki silaha za nyuklia, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Lin Jian amesema jana Jumatatu, akihimiza jumuiya ya kimataifa kuwa macho na kwa uthabiti kupinga kauli kama hizo.

"Kauli hizo ni changamoto ya wazi kabisa kwa utaratibu wa kimataifa wa baada ya vita na mfumo wa kutoeneza silaha za nyuklia, ni tishio kubwa kwa amani na utulivu wa kikanda na kimataifa, na ni hatua ya kurudi nyuma kutoka ahadi ya Japan ya maendeleo ya amani," Lin amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari, akiongeza kuwa hili si jambo la kushawishi hata kidogo kusema kuwa wazo hilo la Japan kumiliki silaha za nyuklia ni "maoni binafsi."

Kwa mujibu wa Lin, Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Japan amekataa kutoa ufafanuzi kuhusu kauli za afisa huyo ambaye ametajwa kuwa mtu wa karibu na Waziri Mkuu Sanae Takaichi. Aidha, amesema, Waziri wa Ulinzi wa Japan baadaye alisema kwamba uwezekano wa Japan kupitia upya kanuni zake za kutokuwa na silaha za nyuklia umeachwa wazi katika siku zijazo.

Lin amesema kwamba kwa miaka mingi, vikundi vya mrengo wa kulia vya Japan vimekuwa vikisukuma mbele uimarishaji wa kijeshi wa nchi hiyo, na azma yao ya kurejesha umilitarizm ni wazi.

"Viongozi wa zamani wa kisiasa wa Japan wamedai kuwa Japan ina uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia. Japan kwa muda mrefu imekuwa ikizalisha na kumiliki akiba ya plutonium inayozidi kwa kiasi kikubwa mahitaji ya matumizi ya kiraia ya nishati ya nyuklia. Japan ni nchi isiyo na silaha za nyuklia lakini yenye uwezo wa kuzalisha plutonium ya daraja la silaha." amesema.

Lin ameeleza kwamba kauli hizo za afisa huyo mwandamizi zinaonyesha wazi juhudi za vikundi vya mrengo wa kulia vya Japan za kujaribu "kurejesha umilitarizm" na "kujipatia tena silaha".

Amesema nyaraka zilizo na nguvu ya kisheria chini ya sheria za kimataifa, zikiwemo za Azimio la Cairo, Tangazo la Potsdam, na Hati ya Kujisalimisha ya Japan, zinaweka wazi kwamba Japan inapaswa kupokonywa silaha kabisa na isidumishe viwanda vinavyoweza kuiwezesha kujipatia tena silaha kwa ajili ya vita.

"Iwapo vikundi vya mrengo wa kulia nchini Japan vitaachwa huru kuendeleza silaha zenye nguvu za kushambulia, au hata kumiliki silaha za nyuklia, italeta maafa tena kwa dunia," ameonya.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha