China na DRC zaimarisha ushirikiano katika mafunzo ya ufundi stadi

(CRI Online) Desemba 23, 2025

Mkutano kati ya China na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuhusu mafunzo ya ufundi stadi umefanyika jana Jumatatu mjini Kinshasa, mji mkuu wa DRC, ukilenga kuimarisha ushirikiano wa pande mbili.

Kwenye hotuba yake wakati wa mafunzo hayo, Waziri wa Mafunzo ya Ufundi Stadi wa DRC Marc Ekila Likombio amesema kuwa elimu ya ufundi na ufundi stadi ina jukumu muhimu katika kuhimiza maendeleo ya viwanda ya nchi hiyo na kuboresha ajira kwa vijana.

Waziri huyo ameeleza nia ya DRC ya kuimarisha ushirikiano na China katika nyanja hiyo, kujifunza kutoka kwenye uzoefu wa China katika mafunzo ya ufundi stadi, uendelezaji ujuzi na ushirikiano kati ya shule na kampuni.

Balozi wa China nchini DRC Zhao Bin amesema DRC iko katika hatua muhimu ya mageuzi ya kijamii na kiuchumi, huku ikiwa na mahitaji yanayoongezeka ya wafanyakazi wenye ujuzi wa ufundi.

Ameongeza kuwa China inaweka umuhimu mkubwa kwenye ushirikiano na DRC katika mafunzo ya ufundi stadi na itaendelea kutoa programu za mafunzo kulingana na mahitaji ya nchi hiyo, haswa katika miundombinu, madini, kilimo, huduma za afya na teknolojia ya kupashana habari.

Aidha Balozi huyo amesema ushirikiano wa kivitendo kati ya China na DRC umepata matokeo halisi, ambapo kampuni za China zimetoa nafasi za ajira za moja kwa moja zaidi ya laki moja nchini DRC na kutekeleza miradi ya uwajibikaji wa kijamii iliyonufaisha jamii zaidi ya 300 za wenyeji.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha