Kituo cha usambazaji bidhaa kilichojengwa na China nchini Tanzania chaboresha biashara ya kikanda Afrika Mashariki

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 23, 2025

Wafanyakazi wakisaidia wateja kwenye duka la bidhaa za  kielektroniki katika Kituo cha Biashara na Usambazaji Bidhaa cha Afrika Mashariki (EACLC) jijini Dar es Salaam, Tanzania, Desemba 19, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Wafanyakazi wakisaidia wateja kwenye duka la bidhaa za kielektroniki katika Kituo cha Biashara na Usambazaji Bidhaa cha Afrika Mashariki (EACLC) jijini Dar es Salaam, Tanzania, Desemba 19, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

DAR ES SALAAM - Kwenye ghorofa ya pili ya Kituo cha Biashara na Usambazaji Bidhaa cha Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo pembezoni mwa jiji la bandari la Dar es Salaam nchini Tanzania, nguo zilizopangwa vizuri zimejaa kwenye rafu, huku wateja wakifika kutoka sehemu mbalimbali za nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kwingineko.

Ayoub Katuga, mfanyabiashara Mtanzania anaonekana mwenye tabasamu, baada ya biashara yake ya jumla ya nguo kupata msukumo mpya ndani ya kituo hicho cha kisasa katika eneo la Ubungo.

"Mazingira haya yamebadilisha kabisa namna tunavyofanya biashara," Katuga amesema, akionyesha chumba cha kuonyesha bidhaa chenye mwanga angavu na mpangilio mzuri.

"Wateja wetu wanafurahia kuja hapa, na hilo pekee linaleta tofauti kubwa," ameyasema hayo kwenye mahojiano ya hivi karibuni na Shirika la Habari la China, Xinhua.

Katuga ni mkurugenzi msimamizi wa Ascon Africa. Alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara wa kwanza wenyeji kufungua duka kwenye kituo hicho, kituo cha biashara kilichojengwa na China kwa lengo la kupunguza vikwazo vya biashara kati ya China, Tanzania na eneo pana la Afrika Mashariki.

"Nilikuja hapa mwezi Agosti na kufungua duka kwenye ghorofa ya chini. Sasa tumepanuka hadi ghorofa ya kwanza kwa kufungua duka jingine jipya, tukilenga biashara ya jumla ya nguo. Ukuaji huu wenyewe unaonyesha maendeleo tuliyoyapata" amekumbushia.

Kikiwa katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, kituo hicho siyo tu soko la kawaida. Kimeundwa kama jukwaa la huduma za biashara na usambazaji bidhaa katika sehemu moja, kinajumuisha vyumba vya kuonesha bidhaa, maghala, uratibu wa usafirishaji, huduma za forodha na za biashara katika sehemu moja.

Kwa Katuga, ambaye wateja wake hutoka Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi na Uganda, kituo hicho kimefungua fursa mpya za biashara.

Amesema jukwaa hilo limeimarisha mnyororo wake wa usambazaji bidhaa na China, ambako bidhaa zake nyingi hutoka.

"Linatuunganisha moja kwa moja na wauzaji Wachina na kuvutia wanunuzi wa kikanda kuja Tanzania. Huo ni muundo mpya wa biashara," amesema.

Kampuni za China pia zinaendelea kujiimarisha kwenye kituo hicho. Miongoni mwa kampuni hizo ni MAFC, inayojihusisha na samani, taa na vifaa vya ujenzi. Baada ya kukarabati chumba chake cha kuonyesha bidhaa mwezi Agosti, kampuni hiyo ilianza rasmi shughuli zake mwezi Oktoba mwaka huu.

"Biashara imekuwa ikiongezeka siku hadi siku," amesema Wang Xinggang, mwakilishi wa kampuni hiyo ya China, akieleza kuwa Tanzania ilichaguliwa kutokana na faida zake bora za kimkakati, ikiwemo idadi kubwa ya watu, ufikiaji wa bahari, utulivu wa kisiasa na uwezekano mkubwa wa maendeleo.

Cathy Wang, meneja mkuu wa EACLC, amesema kwamba kuanzishwa kwa kituo hicho kulitokana na hitaji la kuboresha ufanisi na muundo wa biashara kati ya China na Afrika.

"Lengo letu la awali lilikuwa kujenga jukwaa la biashara lililo rahisi, lenye ufanisi na salama zaidi. Kwa kupunguza pengo la taarifa na gharama kubwa za usafirishaji, tunalenga kuibadilisha biashara ya China na Afrika kutoka uendeshaji uliogawanyika na wa ukubwa mdogo kuelekea mfumo uliopangiliwa na unaotegemea jukwaa." amesema.

Kwa sasa, kituo hicho kinahudumia wafanyabiashara kutoka China na Tanzania, pamoja na nchi jirani kama Kenya, Uganda, Rwanda na Somalia. Bidhaa zilizouzwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi na mashine, bidhaa za kielektroniki, nguo na mahitaji ya kila siku.

Mfanyabiashara akiangalia nguo zinazooneshwa ndani ya chumba cha biashara ya kuuza nguo kwa jumla katika Kituo cha Biashara na Usambazaji Bidhaa cha Afrika Mashariki (EACLC) jijini Dar es Salaam, Tanzania, Desemba 19, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Mfanyabiashara akiangalia nguo zinazooneshwa ndani ya chumba cha biashara ya kuuza nguo kwa jumla katika Kituo cha Biashara na Usambazaji Bidhaa cha Afrika Mashariki (EACLC) jijini Dar es Salaam, Tanzania, Desemba 19, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Cathy Wang, meneja mkuu wa Kituo cha Biashara na Usambazaji Bidhaa cha Afrika Mashariki (EACLC), akizungumza katika  mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua jijini Dar es Salaam, Tanzania, Desemba 19, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Cathy Wang, meneja mkuu wa Kituo cha Biashara na Usambazaji Bidhaa cha Afrika Mashariki (EACLC), akizungumza katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua jijini Dar es Salaam, Tanzania, Desemba 19, 2025. (Xinhua/Emmanuel Herman)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha