China yaitaka Marekani kufuta uamuzi wa kimakosa wa kuweka droni kwenye "orodha yake ya vifaa tishio kwa usalama wa taifa"

(CRI Online) Desemba 24, 2025

Wizara ya Biashara ya China imeitaka Marekani kukomesha vitendo vyake vya kimakosa kuhusu uamuzi wa Kamisheni ya Mawasiliano ya Serikali Kuu ya Marekani (FCC) wa kuongeza droni zilizotengenezwa nje ya nchi na vipuri muhimu kwenye "orodha yake ya vifaa tishio kwa usalama wa taifa".

Msemaji wa wizara hiyo amesema jana Jumanne kwamba China inapinga vikali hatua hiyo na imeutaka upande wa Marekani kufuta hatua husika mara moja.

"Orodha ya vifaa tishio kwa usalama wa taifa" iliyorekebishwa na kutangazwa upya Jumatatu wiki hii, inabainisha vifaa na huduma za mawasiliano zinazochukuliwa kuwa zinaleta tishio lisilokubalika kwa usalama wa taifa wa Marekani, au usalama wa watu wa Marekani.

Kuongezwa kwenye orodha hiyo kunamaanisha kuwa mifumo mipya ya droni zilizotengenezwa nje ya nchi na vipuri muhimu vimepigwa marufuku kupewa idhini ya FCC, na hivyo kupiga marufuku uagizaji na uuzaji wake nchini Marekani.

Msemaji huyo wa China amesema kwamba bila kujali shughuli za kawaida za kibiashara kati ya kampuni za China na Marekani vilevile maombi mazito kutoka kwa wadau wa viwanda vya nchi zote mbili, Marekani imerudia tena kuielezea kwa ujumla dhana ya usalama wa taifa na kutumia vibaya mamlaka ya serikali kukandamiza kampuni za nchi nyingine, zikiwemo kampuni za China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha