China yawasilisha kwa Umoja Mataifa hati yake ya kuidhinisha makubaliano juu ya bioanuwai za baharini

(CRI Online) Desemba 24, 2025

Kwa mujibu wa hati zilizochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Umoja wa Mataifa jana Jumanne, China iliwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hati ya kuidhinisha Makubaliano chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya Bahari juu ya Uhifadhi na Matumizi Endelevu ya Bioanuwai za Baharini za Maeneo yaliyo Nje ya Mamlaka ya Kitaifa siku ya Desemba 15.

Makubaliano hayo ni mkataba muhimu wa kimataifa chini ya mfumo wa Umoja wa Mataifa. Kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya Bahari, yanalenga kuhifadhi na kuwa na matumizi endelevu ya bioanuwai za baharini, yakijikita katika rasilimali za kinasaba za kwenye bahari ya kina kirefu, maeneo yanayolindwa ya baharini, tathmini za athari za mazingira na ujengaji wa uwezo.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya miaka 19 ya majadiliano yaliyohusisha nchi zaidi ya 190. Wakati makubaliano hayo yalipofikia idadi inayohitajika ya nchi kuyaidhinisha ili kuanza kutumika rasmi, Bw. Guterres alikaribisha hatua hiyo, akiielezea kuwa ni "mafanikio ya kihistoria kwa bahari na kwa ushirikiano wa pande nyingi".

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha