Lugha Nyingine
Upanuzi wa mtandao wa reli ya mwendokasi waharakisha maendeleo yenye sifa bora ya China
YINCHUAN - Mwaka unapokaribia kuisha, mtandao wa reli ya mwendokasi wa China umepanuka zaidi kwa kufunguliwa kwa njia kadhaa mpya, hali ambayo imerahisisha usafiri wa umma na kuharakisha maendeleo yenye sifa bora katika maeneo yaliyo kando ya reli hizo.
Takriban saa 4 asubuhi siku ya Jumanne, treni ya mwendokasi No. D4667 iliondoka kutoka Mji wa Baotou wa Mkoa wa Mongolia ya Ndani kuelekea Yinchuan, mji mkuu wa Mkoa Unaojiendesha wa Kabila la Wahui wa Ningxia, kaskazini magharibi mwa China. Safari hiyo kwenye njia mpya imepunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kusafiri kati ya miji hiyo miwili, kutoka zaidi ya saa sita hadi takriban saa 2.5.

Mfanyakazi akikagua treni ya kwanza ya reli ya mwendokasi ya Baotou-Yinchuan kwenye Stesheni ya Reli ya Baotou mjini Baotou, Mkoa Unaojiendesha wa Mongolia ya Ndani, Kaskazini mwa China, Desemba 23, 2025. (Xinhua/Li Zhipeng)
Kwa uwekezaji wa yuan bilioni 54.63 (sawa na dola za Marekani bilioni 7.75), reli hiyo yenye urefu wa kilomita 519 ni sehemu muhimu ya reli ya mwendokasi inayounganisha Beijing na Lanzhou, mji mkuu wa Mkoa wa Gansu, ikikamilisha sehemu ya mwisho kwenye mtandao wa reli ya mwendokasi wa eneo la kaskazini magharibi mwa China.
Siku moja kabla, njia mbili za reli ya mwendokasi katika Mkoa wa Guangdong zilianza kutoa huduma, na kupunguza kwa kiasi kikubwa muda wa kusafiri ndani ya Eneo la Ghuba Kuu ya Guangdong-Hong Kong-Macao. Kufunguliwa kwa njia mpya tarehe 5 Desemba katika mkoa wa Guangxi kusini mwa China kumeongeza njia mpya ya usafiri kati ya China na nchi za ASEAN.
Reli ya Xi'an-Yan'an katika Mkoa wa Shaanxi na reli ya Hangzhou-Quzhou katika Mkoa wa Zhejiang pia zinatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni, na kuboresha muunganisho kwenye eneo la kihistoria la mapinduzi ya China kaskazini mwa Mkoa wa Shaanxi pamoja na eneo la Delta ya Mto Yangtze.
Kufuatia kufunguliwa kwa reli hizo za mwendokasi ifikapo mwisho wa mwaka huu, jumla ya urefu wa mtandao wa reli ya mwendokasi wa China unatarajiwa kuzidi kilomita 50,000.

Picha ikionyesha treni ya mwendokasi ikipita juu ya daraja kwenye reli ya mwendokasi ya Hangzhou-Quzhou katika Mkoa wa Zhejiang, mashariki mwa China, Novemba 20, 2025. (Xinhua/Huang Zongzhi)
Tangu China ilipoanzisha huduma yake ya reli ya mwendokasi mwaka 2008, imejenga mtandao mkubwa zaidi wa reli ya mwendokasi duniani, ukichukua zaidi ya asilimia 70 ya jumla ya reli za mwendokasi duniani.
Kila siku, hadi treni za mwendokasi 10,000 hubeba takriban abiria milioni 16, huku hadi kufikia mwisho wa mwaka 2024, treni hizo zikiwa zimeshasafirisha jumla ya abiria zaidi ya bilioni 22.9.

Mfanyakazi (katikati) akiwasiliana na abiria ndani ya treni ya mwendokasi No. D4667, Desemba 23, 2025. (Xinhua/Li Zhipeng)
Kanyanat In-Aim, mwanafunzi wa Thailand anayesoma Chuo Kikuu cha Ningxia, alitembelea mji wa Xi'an kwa kutumia reli ya mwendokasi wakati wa mapumziko ya majira ya joto.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 alisema muda mfupi wa safari na nauli nafuu ya tiketi hufanya treni za mwendokasi kuwa chaguo la kwanza kwa wanafunzi kama yeye.
"Ni nafuu zaidi kuliko kusafiri kwa ndege, ina ratiba za mara kwa mara, mnyumbuliko mkubwa zaidi na ucheleweshaji mdogo," amesema.
Kwa mujibu wa mipango ya kitaifa ya China, ifikapo mwaka 2035, mtandao wa reli ya mwendokasi wa China utatarajiwa kufikia kilomita 70,000, ukiwa na njia kuu nane zinazounganisha kaskazini na kusini na njia nane zinazounganisha mashariki na magharibi. Mara tu utakapokamilika, mtandao huo utaunganisha miji mikubwa, makundi ya miji, na maeneo muhimu ya kiuchumi nchini kote.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



