Lugha Nyingine
Bandari ya Biashara Huria ya Hainan kuwa lango muhimu la ufunguaji mlango wa kiwango cha juu wa China
BEIJING - Bandari ya Biashara Huria ya Hainan (FTP) itakuwa lango muhimu la ufunguaji mlango wa kiwango cha juu wa China, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Lin Jian amesema jana Jumanne kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akijibu swali kuhusu uzinduzi wa hivi karibuni wa uendeshaji maalum wa forodha kisiwani kote Hainan.
Amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa eneo maalum la kiuchumi la Hainan mwaka 1988 hadi uzinduzi wa hivi karibuni wa uendeshaji maalum wa forodha katika Bandari ya Biashara Huria ya Hainan, kisiwa hicho kimeacha alama muhimu kwenye mchakato wa mageuzi na ufunguaji mlango wa China.
"Kuendeleza Bandari ya Biashara Huria ya Hainan kwa viwango vya juu kumeandikwa kwenye Mapendekezo ya Kamati Kuu ya CPC ya Kuandaa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa ya Kiuchumi na Kijamii, yaliyopitishwa kwenye mkutano wa nne wa wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya CPC," Lin amesema.
Amesema kwamba katika kukabiliana na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika katika uchumi wa dunia, mwitikio wa China ni kutekeleza ahadi yake ya kufungua mlango kwa vitendo halisi, kupambana na kujihami kiuchumi kwa azma thabiti, na kuhimiza uchumi wa dunia ulio wazi.
"Orodha hasi ya China kwa ufikiaji wa uwekezaji wa kigeni imeendelea kupungua, vizuizi vya ufikiaji kwa sekta ya viwanda vimeondolewa kabisa, sera ya kutotoza ushuru kwa asilimia 100 ya bidhaa kutokoa nchi zote zilizo nyuma kimaendeleo (LDCs) ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia na China, na sera kuingia bila visa kwa abiria wanaoingia China na wale wanaokuja kuunganisha ndege kwenda nchi nyingine zimeboreshwa zaidi," amesema.
Ameeleza kwamba kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu, China imeshuhudia kuanzishwa kwa zaidi ya kampuni 60,000 mpya zenye uwekezaji wa kigeni, ongezeko la asilimia 16.9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana. Ameongeza kuwa, jumla ya biashara ya bidhaa ilizidi yuan trilioni 41 (takribani dola za Marekani trilioni 5.81), ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.6 ikilinganishwa na mwaka jana. Aidha, China imeendelea kuongeza upana na kina cha ufunguaji mlango wake na kuonyesha uhimilivu na nguvu hai kwenye biashara.
Msemaji huyo amesema Mkutano wa Kamati Kuu ya Kazi ya Uchumi wa hivi karibuni umebainisha kuendelea kushikilia sera ya kufungua mlango na kuhimiza ushirikiano wa kunufaishana katika maeneo mbalimbali kuwa moja ya majukumu makubwa ya mwaka ujao, akiongeza kuwa China itafungua mlango zaidi, kutoa fursa zaidi za maendeleo na kuingiza kasi mpya kwa ajili ya ustawi wa pamoja duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



