Trump arudia wito wa kuichukua Greenland licha ya upinzani mkali

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 24, 2025

WASHINGTON - Rais Donald Trump wa Marekani amerudia wito wake wa kuichukua Greenland, ambao umesababisha upinzani mkali kutoka Greenland, Denmark na Umoja wa Ulaya.

"Tunaihitaji Greenland kwa ajili ya usalama wa taifa, si kwa madini," Trump aliwaambia waandishi wa Habari Jumatatu kwenye hoteli yake ya mapumziko ya Mar-a-Lago huko Palm Beach, Florida.

Kauli hiyo inatofautiana na kauli ya awali ya utawala wake, ambayo ilisisitiza mchanganyiko wa masuala ya Usalama wa Taifa, Mkakati wa eneo la Aktiki, pamoja na uwezekano wa kuwepo kwa madini muhimu na rasilimali asili kama sababu za maslahi ya Marekani.

Siku ya Jumapili, Trump alitangaza uteuzi wa Gavana wa Louisiana Jeff Landry kuwa Mjumbe wake Maalum wa Greenland.

"Ni lazima tuipate (Greenland) na yeye (Landry) alitaka kuongoza jukumu hilo," Trump alisema.

Akijibu, Landry aliandika kwenye mtandao wa kijamii X kwamba nafasi hiyo ya mjumbe maalum itakuwa "ya kujitolea kwa lengo la kuifanya Greenland kuwa sehemu ya Marekani."

Greenland, koloni la zamani la Denmark, ilipewa utawala wa ndani mwaka 1979. Mwaka 2009, Denmark ilipitisha Sheria ya kujitawala ya Greenland, ambayo ilipanua mamlaka ya kisiwa hicho katika mambo yake ya ndani. Hata hivyo, Denmark bado inashikilia mamlaka juu ya sera ya kigeni, ulinzi na usalama ya Greenland, kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Denmark.

Uteuzi wa Trump wa mjumbe maalum wa Greenland umezua hisia kali za kidiplomasia kutoka Greenland, Denmark na Umoja wa Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Lars Lokke Rasmussen alisema Jumatatu kwamba atamwita Balozi wa Marekani nchini Denmark Kenneth Howery kufuatia uteuzi huo.

Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen na Waziri Mkuu wa Greenland Jens-Frederik Nielsen walisema Jumatatu katika taarifa ya pamoja kwamba wanatarajia Marekani kuheshimu "ukamilifu wa ardhi na mamlaka yao ya pamoja."

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha