Mji mkuu wa Somalia waanza uchaguzi wa kwanza wa moja kwa moja katika zaidi ya miongo mitano

(CRI Online) Desemba 26, 2025

Zaidi ya wapiga kura 500,000 katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, walipiga kura siku ya Alhamisi katika uchaguzi wa manispaa unaoonekana kama hatua muhimu ya kuelekea uchaguzi wa kwanza wa moja kwa moja wa kitaifa nchini humo katika zaidi ya miongo mitano, uliopangwa kufanyika mwaka 2026.

Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi na Mipaka ya Somalia (NIEBC) ilisema wagombea wapatao 1,604 kutoka vyama 20 vya siasa wanawania nafasi 390 katika mabaraza ya wilaya huko Mogadishu, katika kura inayodhaniwa kuwa muhimu katika kuvunja mfumo wa kisiasa wa muda mrefu wa kiukoo nchini humo.

Kura hiyo inaashiria uchaguzi wa kwanza wa moja kwa moja kufanyika Mogadishu katika miongo kadhaa. Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi, vituo 523 vya kupigia kura katika wilaya 16 vilifunguliwa saa 12 kamili asubuhi kwa saa za huko na kufungwa saa 12 jioni, huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa leo Ijumaa.

Kabla ya kupiga kura, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema uchaguzi wa manispaa ni hatua muhimu kwa ajili ya kufufua serikali na usalama wa mji mkuu, akiwahimiza wapiga kura walioandikishwa kutumia haki zao za kikatiba.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha