Lugha Nyingine
China yatoa msaada wa pikipiki kwa polisi wa Ethiopia
Ubalozi wa China umetoa msaada wa makumi ya pikipiki kwa Tume ya Polisi ya Shirikisho la Ethiopia ili kuunga mkono kazi ya usimamizi wa mawasiliano ya barabarani na usalama.
Siku ya Jumanne, katika makao mkuu ya tume hiyo mjini Addis Ababa, Ethiopia, pikipiki hizo zilikabidhiwa rasmi. Mkuu wa polisi wa Ethiopia, Kamishna Jenerali Demelash Gebremichael, maofisa wengi waandamizi wa usalama wa Ethiopia na wanadiplomasia wa China walishiriki kwenye hafla ya makabidhiano.
Kukabidhiwa kwa pikipiki hizo za kisasa na sare za polisi kunatarajiwa kuongeza uwezo wa polisi wa Ethiopia katika kulinda watu wakubwa, kutoa huduma za uongozaji na kusimamia trafiki kwenye barabara kuu.
Tume hiyo imesisitiza kuwa, nchi za Afrika Mashariki zina uwezo unaozidi kuongezeka wa kuandaa shughuli za ngazi ya juu za kimataifa, kikanda na kitaifa, na pikipiki hizi mpya zitafanya kazi muhimu katika kuwapokea na kuwaongoza viongozi na wageni wa nchi za nje wanaoshiriki kwenye shughuli hizo.
Kaimu balozi wa China nchini Ethiopia Sun Mingxi alipongeza juhudi za polisi wa Ethiopia katika kulinda usalama na haki halali za mashirika ya China na watu wao wanaoishi nchini humo.
Inatarajiwa kuwa msaada huo utasaidia kuhakikisha utaratibu mzuri wa mawasiliano barabarani wakati Addis Ababa inapoandaa shughuli muhimu. Ukiwa mwenyeji wa makao makuu ya Umoja wa Afrika, Addis Ababa kila mwaka unaandaa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika na mikutano mingine ya ngazi ya juu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



