Lugha Nyingine
China kuendelea kufanya juhudi kurejea amani kati ya Thailand na Cambodia

(Picha/Xinhua)
KUNMING - China itaendelea kufanya juhudi kurejea amani kati ya Thailand na Cambodia na inapenda kutoa msaada wa kibinadamu kwa wale wanaohitaji msaada katika nchi zote mbili, amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi mjini Yuxi, Mkoani Yunnan, Kusini Magharibi mwa China jana Jumapili wakati akikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Thailand Sihasak Phuangketkeow.
Kufuatia kusainiwa kwa taarifa ya pamoja ya kukubaliana juu ya kusimamisha mapigano, mawaziri wa mambo ya nje wa Cambodia na Thailand wanaongoza ujumbe kukutana mkoani Yunnan kuanzia Desemba 28 hadi 29 kwa mwaliko wa Wang.
Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, amesema ikiwa ni jirani na rafiki wa nchi zote mbili, China haitaki kuona Thailand na Cambodia zikirudi kwenye vita na inatumai zaidi kuona urafiki kati yao ukirejeshwa.
"Inaaminika kwamba ilimradi tu Thailand na Cambodia zinawasiliana kwa msingi wa usawa na kusonga mbele pamoja, hakutakuwa na vizuizi visivyoweza kushindwa," ameongeza.
Amesema China itaendelea kuiunga mkono ASEAN katika kutekeleza jukumu lake stahiki, inapenda kutoa msaada kwa ujumbe wa uangalizi wa ASEAN katika kufuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano.
Kwa upande wake Sihasak amesifu sana juhudi za China katika kupatanisha mgogoro huo kati ya Thailand na Cambodia kwa njia ya Asia, akisema kuwa makubaliano hayo ya kusimamisha mapigano yaliyosainiwa hivi karibuni kati ya Thailand na Cambodia yanaashiria mwanzo mpya.
"Matumizi ya nguvu kamwe si chaguo la Thailand linapokabiliwa na mizozo na majirani wake," Sihasak amesema, akiongeza kuwa Thailand imejitolea kufanikisha usimamishaji mapigano endelevu na kufikia amani ya kweli.
"Tuna nia ya kutazama mbele na kusonga mbele, kuimarisha mawasiliano na Cambodia kupitia njia za pande mbili, na kwa udhati, hatua kwa hatua kurejesha mawasiliano, kujenga upya hali ya kuaminiana, kurekebisha uhusiano wa pande mbili, na kulinda amani na utulivu wa mipaka kati ya nchi hizo mbili na kanda," waziri huyo wa mambo ya nje amesema.

(Picha/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



