China yapinga Israel kutambua Somaliland

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 30, 2025

BEIJING - Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema mjini Beijing jana Jumatatu kwamba China inapinga kithabiti Israel kutambua rasmi Somaliland kuwa "nchi huru yenye mamlaka" na makubaliano ya "kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia" nayo.

Lin amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari, akisema China inaunga mkono kithabiti mamlaka ya nchi, umoja na ukamilifu wa ardhi ya Somalia, na inapinga vitendo vyovyote vya kuharibu ukamilifu wa ardhi ya Somalia.

"China imeona kuwa serikali ya shirikisho ya Somalia mara moja ilitoa taarifa ikipinga hatua hiyo, na jumuiya za kikanda ikiwa ni pamoja na Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Baraza la Ushirikiano la Ghuba, Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu, na Mamlaka ya Kiserikali juu ya Maendeleo ya Afrika Mashariki pia zimeelezea malalamiko makali na kulaumu vikali," Lin amesema.

Amesema kwa mujibu wa nia na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, Somaliland ni sehemu isiyogawanyika ya ardhi ya Somalia.

Lin amesema suala la Somaliland ni jambo la ndani kabisa la Somalia na linapaswa kutatuliwa na watu wa Somalia kwa namna ambayo inaendana na hali halisi na katiba yao ya nchi.

Pia amesisitiza kwamba nchi zilizo nje ya eneo hilo zinapaswa kuacha uingiliaji usiofaa na nchi yoyote haipaswi kuchochea au kuunga mkono nguvu ya mafarakano ndani ya nchi nyingine kwa maslahi yake binafsi.

"Tunauhimiza utawala wa Somaliland kutambua hali halisi ilivyo sasa, na kuacha mara moja shughuli za kujitenga na kushirikiana na vikundi vya nje," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha