Lugha Nyingine
China ni injini muhimu ya ukuaji wa biashara duniani: Afisa wa UNCTAD

Picha hii ikionyesha mwonekano wa Kituo cha Maonyesho na Mikutano cha Kitaifa (Shanghai), ukumbi mkuu wa Maonyesho ya nane ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) mjini Shanghai, mashariki mwa China, Novemba 10, 2025. (Xinhua/Wang Xiang)
GENEVA - Huku hali ya kutokuwa na uhakika na ongezeko la hali ya kujihami zikiendelea kuathiri uchumi duniani, China inaendelea kuwa injini muhimu ya biashara na ukuaji wa uchumi duniani, Luz Maria de la Mora, Mkurugenzi wa Idara ya Biashara na Bidhaa za Kimataifa katika Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) amesema.
Kwenye mahojiano ya hivi karibuni na Shirika la Habari la China, Xinhua, de la Mora ameonya kwamba mabadiliko katika sera ya ushuru ya Marekani tangu mwanzo wa mwaka huu yameongeza kwa kiasi kikubwa hali ya kutokuwa na uhakika kwa kiasi kikubwa katika biashara na uwekezaji wa kimataifa.
Kwa mujibu wa de la Mora, Marekani imepandisha wastani wa viwango vya ushuru kutoka asilimia 2.6 mwanzoni mwa mwaka huu hadi asilimia 17.9 kwa sasa.
"Aina hiyo ya kutokuwa na uhakika kwa kawaida huathiri wawekezaji, washirika wa biashara, na namna minyororo ya usambazaji inavyofanya kazi," amesema, akiongeza kuwa uvurugaji huo si tu unaathiri uagizaji bidhaa wa Marekani na biashara ya dunia lakini pia unadhoofisha mchango wa biashara katika ukuaji wa uchumi kwa ujumla.
Akiangalia siku za baadaye, de la Mora amesema ukuaji wa uchumi duniani unatarajiwa kupungua zaidi. "Tukielekea mwaka 2026, tunatarajia kuona kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia," amesema, akiongeza kuwa mwenendo huo tayari umeonekana dhahiri katika mwaka mzima wa 2025.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Biashara na Maendeleo ya UNCTAD ya 2025, ukuaji wa uchumi duniani unakadiriwa kushuka kutoka asilimia 2.9 mwaka 2024 hadi asilimia 2.6 mwaka 2025, na kubakia katika kiwango hicho takribani mwaka 2026, kiwango kilicho chini ya wastani wa kabla ya janga la COVID wa asilimia takriban 3.
De la Mora amekadiria kwamba vichocheo vikuu vya ukuaji wa biashara mwaka 2026 vitatarajiwa kutokea zaidi kutoka Nchi za Kusini.
Pia amezungumzia sera ya kutotoza ushuru ya China kwa nchi za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China, ni sehemu ya juhudi muhimu za kuhakikisha kuwa biashara inaendelea kuwa injini ya ukuaji.
Akiangalia mwaka 2026, de la Mora ameonya kwamba hali ya kutokuwa na uhakika katika biashara ya kimataifa huenda ikaendelea, kwani kanuni za biashara ya pande nyingi zinaendelea kukumbwa na changamoto kutoka kwa wadau wakuu wanaoweka kipaumbele kwenye masuala ya kitaifa au ya ndani.

Picha hii iliyopigwa Januari 2, 2024, ikionyesha meli ya makontena inayoitwa "WAN HAI 357" ikitia nanga kwenye Bandari ya Dalian katika Mkoa wa Liaoning, kaskazini mashariki mwa China. (Liaoning Port Group/Handout kupitia Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



