China yapinga vikali Israel kuitambua Somaliland kama nchi huru

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 31, 2025

Sun Lei (katikati), Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, akizungumza kwenye mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu yake mjini New York, Desemba 29, 2025. (Xinhua/Zhang Fengguo)

UMOJA WA MATAIFA - China inapinga vikali hatua ya Israel kuitambua Somaliland, eneo lililojitenga la Somalia, kuwa nchi huru, hayo yamesemwa na Sun Lei, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, kwenye mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama uliofanyika Jumatatu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

"Hatua ya Israel ya kuitambua rasmi Somaliland kuwa nchi huru imeongeza mvutano zaidi katika Pembe ya Afrika, na kusababisha ukosoaji na lawama kali kutoka kwa mashirika ya kikanda na nchi za kanda hiyo," amesema Balozi Sun.

Balozi Sun amesema kuheshimu mamlaka na ukamilifu wa ardhi wa nchi ni kanuni ya msingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa na msingi dhabiti wa sheria za kimataifa na uhusiano wa kimataifa, ambao nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa lazima zizingatie na kuzifuata kikamilifu.

"Somaliland ni sehemu isiyotengeka ya Somalia. China inaunga mkono bila kuyumba mamlaka, umoja na ukamilifu wa ardhi ya Somalia, na inapinga kitendo chochote cha kuigawa nchi hiyo. China siku zote imesisitiza kwamba suala la Somaliland ni jambo la ndani la Somalia," amesema, akiongeza kuwa nchi zilizo nje ya eneo hilo zinapaswa kuacha kuingilia kati masuala hayo bila msingi wowote.

"China inaisihi Israeli kutenda kwa kuwajibika, kufuata kikamilifu Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, kusikiliza sauti ya jumuiya ya kimataifa, kuchukua hatua za kurekebisha mara moja kitendo chake, na kuondoa athari zake mbaya mapema iwezekanavyo," amesema Balozi Sun.

Ameongeza kuwa China pia inazitaka mamlaka za Somaliland kuwa na uelewa sahihi wa hali ilivyo, kuacha mara moja shughuli za kujitenga na ushirikiano na nguvu za nje, na kurudi kwenye njia ya mazungumzo na serikali ya shirikisho ya Somalia mapema iwezekanavyo.

"Kwa kuwa Somalia iko katika wakati muhimu wa mpito wa kisiasa na usalama, jumuiya ya kimataifa inapaswa kuendelea kuisaidia katika kuimarisha uwezo wa kupambana na ugaidi, kuendeleza mazungumzo ya kisiasa, na kukuza umoja wa kitaifa," amesisitiza Balozi Sun.

“Ikiwa ni rafiki mwaminifu wa Somalia na nchi za kanda hiyo, China itaendelea kuunga mkono bila kuyumba mamlaka, umoja na ukamilifu wa ardhi ya Somalia, kushikilia haki na usawa, na kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya amani, utulivu, maendeleo na ustawi nchini Somalia na kanda hiyo,” amesema. 

Baraza la Usalama likifanya mkutano wa dharura kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Desemba 29, 2025. (Xinhua/Zhang Fengguo)

Baraza la Usalama likifanya mkutano wa dharura kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Desemba 29, 2025. (Xinhua/Zhang Fengguo)

Sun Lei (katikati, mbele), naibu mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, akizungumza kwenye mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Desemba 29, 2025. (Xinhua/Zhang Fengguo)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha