A3+ zalaani Israeli kuitambua Somaliland kuwa nchi huru

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 31, 2025

Balozi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa Abukar Dahir Osman (katikati, mbele) akizungumza katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Desemba 29, 2025. (Xinhua/Zhang Fengguo)

Balozi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa Abukar Dahir Osman (katikati, mbele) akizungumza katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Desemba 29, 2025. (Xinhua/Zhang Fengguo)

UMOJA WA MATAIFA – Nchi tatu za Afrika wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa -- Algeria, Sierra Leone, na Somalia -- pamoja na Guyana, ambazo kwa pamoja zinajulikana kwa jina la A3+, zimelaani vikali hatua ya Israeli kuitambua Somaliland kuwa nchi huru.

"A3+ inalaani vikali hatua za Israeli dhidi ya umoja na ukamilifu wa ardhi ya Somalia kwa kulitambua kuwa nchi huru eneo la kaskazini magharibi mwa Somalia, linalotambulika kwa jina la Somaliland," imesema A3+ kwenye taarifa ya pamoja katika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama.

Somaliland, eneo lililojitenga la Somalia, "halina uwezo kisheria wa kuingia katika makubaliano au mpango au utambuzi wowote na nchi nyingine," imesema taarifa hiyo iliyosomwa na Balozi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa Abukar Dahir Osman kwa niaba ya A3+, ikiongeza kuwa makubaliano yoyote ya aina hiyo yaliyodaiwa kufikiwa hayana nguvu za kisheria na ni batili.

Taarifa hiyo imesema kwamba hatua hiyo ya Israel kuutambua uhuru wa Somaliland unakiuka moja kwa moja wa Katiba ya Umoja wa Mataifa, kanuni za msingi za Umoja wa Afrika, na unavunja msingi wa sheria za kimataifa.

"Kitendo hiki cha uchokozi kinalenga kuchochea mgawanyiko wa ardhi ya Somalia ... na kinavuruga utulivu katika Pembe ya Afrika, Pembe nzima ya Afrika, na eneo la Bahari Nyekundu. Kinapaswa kukataliwa na kulaaniwa vikali na nchi zote wanachama (wa Umoja wa Mataifa). Kwa hivyo, A3+, inakataa tangazo hili la Israel na inatoa wito wa kufutwa mara moja," imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia inazitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zichukue msimamo mmoja na wenye kuongozwa na kanuni dhidi ya hatua hii haramu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, A3+ inakataa kabisa hatua yoyote inayolenga kulazimisha uhamishaji wa Wapalestina kutoka katika ardhi yao kwenda nchi nyingine, ikiwemo jaribio lolote la Israeli la kuwahamisha watu wa Palestina kutoka Gaza hadi Somaliland.

"Kitendo hiki si tu ni kinyume cha sheria, bali pia ni cha kulaumiwa vikali kimaadili. A3+ haitakubali wala kuruhusu matumizi haramu ya ardhi yoyote, achilia mbali ardhi ya nchi huru yenye mamlaka, ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa," imesema taarifa hiyo.

"Vitendo vya Israeli si tu kwamba vimeweka mfano hatari lakini pia vinatishia sana amani na usalama wa kikanda na kimataifa," imesema taarifa hiyo. 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha