Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping wa China atoa salamu za mwaka mpya wa 2026

(Picha/CRI)
Katika mkesha wa mwaka mpya, rais Xi Jinping wa China ametoa hotuba ya salamu za mwaka mpya wa 2026 kupitia Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG) na mtandao wa Internet. Ifuatayo ni hotuba hiyo:
Hamjambo! Wakati wa zamani umepita huku maisha yakifungua ukurasa mpya. Wakati mwaka mpya unawadia, mimi nikiwa hapa Beijing, napenda kuwapa salamu za mwaka mpya.
Mwaka 2025 ni mwaka uliokamilisha “Mpango wa 14 wa Maendeleo ya Uchumi na Jamii ya Miaka Mitano”. Katika miaka mitano iliyopita, tulifanya kazi kwa bidii na kusonga mbele kwa ushupavu. Tulifanikisha malengo yote yaliyowekwa kwa kushinda magumu na changamoto mbalimbali, na kupiga hatua madhubuti katika safari mpya ya kujenga mambo ya kisasa yenye umaalumu wa China. Pato la taifa la nchi yetu ilivunja rekodi moja baada ya nyingine, mwaka huu inakadiriwa kufikia renminbi yuan trilioni 140. Nguvu ya nchi yetu ya uchumi, sayansi na teknolojia, ulinzi wa nchi, na nguvu ya jumla ya nchi imepanda katika ngazi mpya. Mito na milima ya kijani imekuwa mandhari ya kupendeza, na hisia ya watu ya kupata ustawi, furaha, na usalama inaendelea kuongezeka. Tumepata mafanikio hayo kwa kukabiliana na matatizo yasiyoshuhudiwa hapo awali. Kazi ngumu na kujitolea kwa kila mtu inaijenga China yenye ustawi. Ningependa kuwapongeza wachapa kazi wote waliofanya juhudi kubwa.
Mwaka huu, mambo yasiyosahaulika ni kwamba tumeadhimisha kwa heshima kubwa miaka 80 ya ushindi wa vita ya watu wa China dhidi ya uvamizi wa Japan na ushindi wa vita ya dunia dhidi ya Ufashisti, na tumeweka Siku ya Kumbukumbu ya Taiwan kujitoa kwenye ukoloni wa Japan. Sherehe kubwa za kitaifa zilifanyika kwa fahari, na utukufu wa ushindi umeandikwa milele katika historia, ukiwahamasisha Wachina wote kukumbuka historia, kukumbuka mashujaa waliojitolea mhanga, kuthamini amani, na kuanzisha mustakabali, na pia kukusanya nguvu kuu ya kufanikisha ustawishaji mkubwa wa taifa la China.
Tumetoa tija kwa maendeleo yenye ubora wa juu kupitia uvumbuzi. Teknolojia na sekta za uchumi vimeunganishwa kwa kina zaidi, na matokeo ya uvumbuzi yamejitokeza kwa kasi. Mifumo mikubwa ya AI imeibuka kwa wingi na kuwa na maendeleo, utafiti wa kujitegemea wa chipu umepata mafanikio mapya, na China imekuwa moja ya nchi zenye kasi kubwa zaidi ya ongezeko la nguvu za uvumbuzi duniani. Chombo cha Utafiti wa anga ya juu cha Tianwen-2 kilianza safari yake ya “kufuatilia nyota”, mradi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya maji wa Yaxia ulianza kujengwa, na manowari ya kwanza ya kubeba ndege iliyozatitiwa kwa mfumo wa ulinzi wa umemesumaku ilianza kufanya kazi rasmi kwa jeshi. Roboti zenye umbo la binadamu zilionyesha "mtindo wa kungfu", na uendeshaji wa droni umeonesha fashifashi murua ya kuvutia angani. Uvumbuzi umeleta nguvu mpya za uzalishaji na kufanya maisha ya watu yawe na rangi na uzuri zaidi.
Tulitumia utamaduni kurutubisha maskani ya raha starehe kwa watu, watu wamekuwa na shauku zaidi kwa mabaki ya kale ya kitamaduni, makumbusho, na mali za urithi wa utamaduni usioshikika. Sehemu moja ya kivutio cha utamaduni ya China iliongezwa kwenye Orodha ya Mali ya Urithi wa Dunia. Alama za utamaduni kama vile Wukong na Nezha zimekuwa maarufu duniani. Watu wa kizazi kipya wameanza kuona utamaduni wa kijadi wa China kama aina bora zaidi ya kujieleza kwa uzuri. Sekta za utamaduni na utalii zilistawi. Michezo ya soka ya "ligi kuu" katika miji na vijiji vyetu imewavutia mashabiki wengi. Michezo ya barafu na theluji iliamsha shauku ya watu katika msimu wa baridi. Mila sasa inakumbatia usasa, na utamaduni wa China unazidi kung'aa kwa uzuri.
Tumejenga kwa pamoja na kufurahia kwa pamoja maisha mazuri. Wakati nilipotembelea mikoa ya Xizang na Xinjiang kuhudhuria shughuli za sherehe, kutoka nyanda za juu za theluji hadi maeneo ya kaskazini na kusini mwa Milima Tianshan, nimeona watu wa makabila mbalimbali wameshikamana kwa mikono na mioyo, na kukumbatiana kwa karibu kama mbegu za komamanga, wakionyesha upendo wao kwa taifa na kusifu maisha ya furaha kupitia skafu nyeupe za khata na nyimbo na ngoma zenye uchangamfu. Kazi zinazohusu maisha ya wananchi hazina jambo dogo. Katika mwaka uliopita, makundi ya watu walioajiriwa au waliojiajiri katika majukwaa mbalimbali ya mtandaoni wamepata uhakikisho zaidi wa haki na maslahi, miradi ya maboresho ya makazi au miundombinu kulingana na mahitaji ya wazee imetoa urahisi kwa maisha ya wazee, na familia zenye watoto wachanga zimeongezewa ruzuku ya Yuan 300 kila mwezi. Kama kila familia ndogo ikifurahia maisha ya kila siku, basi familia yetu kubwa ya China itazidi kustawi siku hadi siku.
Tutaendelea kufungua mlango na kukumbatia dunia. Mkutano wa Kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), na Mkutano wa Kilele wa Wanawake Duniani ulifanyika kwa mafanikio, uendeshaji maalumu wa forodha umeanza kufanyika katika Bandari ya Biashara Huria ya Kisiwa cha Hainan. Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ufanisi zaidi, China imetangaza duru mpya ya mchango wa kujitolea kupunguza utoaji wa kaboni. Kufuatia Mapendekezo Matatu, nilitoa Pendekezo la Usimamizi wa Dunia, kwa lengo la kuhimiza uundaji wa mfumo wa usimamizi wa dunia ulio wa haki na wenye mantiki zaidi. Katika dunia ya leo ambayo mabadiliko na machafuko vimechangamana, baadhi ya maeneo bado yanakumbwa na vita. China siku zote imekuwa ikisimama katika upande sahihi wa historia, na inapenda kushirikiana na nchi mbalimbali katika kuhimiza amani na maendeleo ya dunia, na kusukuma mbele ujenzi wa Jumuiya ya Binadamu yenye Mustakbali wa Pamoja.
Si muda mrefu uliopita, nilihudhuria sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Taifa zilizofanyika kwa juhudi za pamoja za mikoa mitatu ya Guangdong, Hong Kong na Macao, hali iliyokuwa ya kutia moyo. Tunatakiwa kutekeleza kithabiti na kikamilifu sera ya “Nchi Moja, Mifumo Miwili”, kuunga mkono mikoa ya Hong Kong na Macao kushirikishwa vizuri zaidi katika mambo makuu ya maendeleo ya nchi, na kudumisha utulivu na ustawi wa muda mrefu. Wachina wa kando mbili za Mlango-Bahari wa Taiwan wana undugu wa damu, na mwelekeo mkuu wa kihistoria wa China kutimiza muungano wa taifa hauzuiliki!
Nchi haiwezi kuwa na nguvu bila ustawi wa Chama. Tumefanya mafunzo ya misingi ya kutekeleza kwa kina nidhamu nane za Kamati Kuu ya Chama. Tumejenga uaminifu kwa kutimiza ahadi, na kushughulikia mambo ya Chama kwa nidhamu kali. Tumeadhibu vitendo vibaya ili kujiendeleza. Maadili ya Chama na serikali yanaboreshwa siku hadi siku. Tunapaswa kushikilia nia ya awali na majukumu yetu, kufanya juhudi bila kusitasita kwa muda mrefu, na kuendelea kujibu “swali la Yaodong” wakati wa Yan’an, ili kutekeleza vizuri majukumu yetu ya zama hizi kwa wananchi.
Mwaka 2026 utakuwa ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa Mpango wa 15 wa Maendeleo ya Uchumia na Jamii ya Miaka Mitano. Wale wanaoanza na lengo kubwa hupata mafanikio makubwa, na wale wanaofanikiwa, hupanga vizuri tangu mwanzo. Ni lazima kulenga kwa usahihi malengo yetu, kuimarisha imani na kutumia fursa, kuhimiza kwa uthabiti maendeleo yenye sifa bora, kuhimiza zaidi mageuzi na ufunguaji mlango katika sekta zote, kuhimiza ustawi wa pamoja wa watu wote, na kufungua ukurasa mpya wa muujiza wa China.
Tunatafuta ndoto katika milima na bahari, na umbali hauwezi kutuzuia. Safari ni ndefu, lakini tunasonga mbele kwa hatua kubwa. Tuwe na ujasiri wa kufanya kazi kwa bidii na nguvu ya kusonga mbele kama farasi wengi wanaokimbia, kudumisha nia ya kufanya juhudi bila kuchoka, kujitahidi kutimiza ndoto na maisha bora kwa pamoja, na kugeuza matarajio yetu makubwa yawe hali halisi nzuri.
Jua la mwaka mpya linakaribia kuchomoza. Nalitakia taifa letu mandhari nzuri, ardhi yenye rutuba, na mustakabali mzuri! Nawatakia ninyi nyote furaha moyoni, mafanikio ya kazi, na mtimize ndoto zote!
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



