Lugha Nyingine
Maduro akamatwa na kupelekwa nje ya Venezuela katika shambulizi kubwa la Marekani

Picha hii iliyopigwa Januari 3, 2026 ikionyesha magari ya kijeshi karibu na Ikulu ya rais mjini Caracas, Venezuela. (Xinhua)
WASHINGTON/CARACAS - Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba Marekani imeishambulia Venezuela na kumkamata Rais Nicolas Maduro, ambaye pamoja na mkewe alisafirishwa kwa ndege nje ya nchi hiyo.
"Marekani imefanikiwa kutekeleza shambulizi kubwa dhidi ya Venezuela na kiongozi wake, Rais Nicolas Maduro, ambaye pamoja na mkewe, amekamatwa na kusafirishwa nje ya Nchi," Trump ameandika jana Jumamosi kwenye Mtandao wa kijamii Truth Social, akiongeza kuwa operesheni hiyo "imefanywa kwa ushirikiano na Vyombo vya Utekelezaji wa Sheria vya Marekani."
Ndege zilizokuwa zikiruka kwenye mwiniko wa chini zilionekana, huku mawingu ya moshi yakionekana kufuatia sauti kubwa za mlipuko karibu na saa 8:00 usiku (06:00 GMT) Jumamosi mjini Caracas, hali iliyowafanya watu kukimbilia mitaani na kusababisha kukatika kwa umeme kwa muda katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu, yakiwemo kambi moja ya kijeshi.
Muda mfupi baada ya shambulizi kuanza, serikali ya Venezuela ililaani "uvamizi wa kijeshi" wa Marekani, ikiongeza kuwa shambulizi hilo lililenga maeneo ya kiraia na kijeshi katika angalau majimbo manne ya nchi hiyo.
Kufuatia tangazo la Trump, Makamu Rais wa Venezuela Delcy Rodriguez amesema kupitia TV ya serikali kwamba serikali haijui Maduro na mkewe waliko, akiongeza, "Tunataka uthibitisho wa uhai."
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Vladimir Padrino Lopez amesema katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba jeshi la Marekani mapema Jumamosi lilishambulia maeneo ya mijini kote Venezuela kwa makombora na roketi.
"Uvamizi huu ni dharau kubwa zaidi ambayo nchi imewahi kukumbana nayo," Padrino amesema. "Mbali na madai ya kupambana na ugaidi wa dawa za kulevya, hatua hii ya kusikitisha inalenga kulazimisha mabadiliko ya utawala."
Waziri huyo ametangaza kutumwa kwa vikosi vya kijeshi kote nchini ili kupambana na uwepo wa wanajeshi wa kigeni.
Gazeti la New York Times liliripoti Jumamosi, likimnukuu afisa wa serikali ya Marekani, kwamba hakukuwa na majeruhi au vifo kwa upande wa Marekani katika operesheni hiyo ya kijeshi dhidi ya Venezuela.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani mapema Jumamosi asubuhi ilipiga marufuku ndege za Marekani kuruka katika mwinuko wowote wa anga ya Venezuela kufuatia ripoti za milipuko mjini Caracas, ikitaja "hatari za usalama wa safari za anga kutokana na operesheni za kijeshi zinazoendelea."
Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Marekani imeendelea kudumisha uwepo mkubwa wa kijeshi katika eneo la Karibiani, ikiwemo manowari ya kubeba ndege USS Gerald R. Ford, na wanajeshi wapatao 15,000, wengi wao wakiwa karibu na pwani ya Venezuela, wakidaiwa kupambana na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya -- madai ambayo Venezuela imeyakanusha, ikilisema ni kisingizio cha kuleta mabadiliko ya utawala nchini humo.

Picha hii iliyopigwa Januari 3, 2026 ikionyesha eneo karibu na Ikulu ya rais mjini Caracas, Venezuela. (Xinhua)

Picha hii iliyopigwa Januari 3, 2026 ikionyesha magari ya kijeshi karibu na Ikulu ya rais mjini Caracas, Venezuela. (Xinhua)

Picha hii iliyopigwa Januari 3, 2026 ikionyesha eneo karibu na Ikulu ya rais mjini Caracas, Venezuela. (Xinhua)

Picha hii iliyopigwa Januari 3, 2026 ikionyesha eneo karibu na Ikulu ya rais mjini Caracas, Venezuela. (Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



