Lugha Nyingine
Wang Yi azungumza kuhusu hali ya Venezuela: China siku zote inapinga nchi moja kulazimisha matakwa yake kwa nyingine

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akiwa anafanya Duru ya Saba ya Mazungumzo ya Kimkakati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Pakistan na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Mohammad Ishaq Dar mjini Beijing, mji mkuu wa China, Januari 4, 2026. (Xinhua/Jin Liangkuai)
BEIJING - China siku zote inapinga matumizi au tishio la nguvu, vilevile nchi moja kulazimisha matakwa yake kwa nchi nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema alipokuwa akizungumzia hali ya Venezuela katika Duru ya Saba ya Mazungumzo ya Kimkakati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Pakistan na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Mohammad Ishaq Dar iliyofanyika mjini Beijing Jumapili.
Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amesema hali ya sasa ya kimataifa imekuwa tete zaidi na changamana, huku ukandamizaji wa upande mmoja ukizidi kuongezeka.
Amesema mabadiliko ya ghafla ya hali nchini Venezuela yamevutia ufuatiliaji mkubwa wa jumuiya ya kimataifa.
"Hatukuwahi kamwe kuamini kwamba nchi yoyote inaweza kuchukua jukumu la polisi wa dunia, wala hatukubaliani kwamba nchi yoyote inaweza kujidai kuwa jaji wa kimataifa," Wang amesema, akiongeza kuwa mamlaka na usalama wa nchi zote unapaswa kulindwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Amesema China ina nia ya kushirikiana na jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Pakistan, ili kushikilia bila kuyumbayumba Katiba ya Umoja wa Mataifa, kulinda msingi wa maadili ya kimataifa, kuheshimu usawa wa mamlaka za nchi zote, na kwa pamoja kulinda amani na maendeleo ya dunia, pamoja na kuhimiza ujenzi wa jumuiya ya binadamu yenye mustakabali wa pamoja.
Kuhusu uhusiano kati ya China na Pakistan, Wang amesema China inatumai ziara hiyo itaanzisha maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Huku akisema kuwa ushirikiano wa hali zote wa kiwenzi na kimkakati kati ya China na Pakistan umekuwa nguzo muhimu ya utulivu wa kikanda na hata wa kimataifa, Wang amesema China inapenda kushirikiana na Pakistan kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya wakuu wa nchi hizo mbili katika mwaka mpya, na kusukuma mbele ujenzi wa jumuiya ya China na Pakistan yenye mustakabali wa pamoja.
Kwa upande wake, Dar amewasilisha salamu za dhati kutoka kwa viongozi wa Pakistan kwa viongozi wa China, na kutoa pongezi kwa CPC kwa kupitisha mapendekezo ya Mpango wa 15 wa Miaka Mitano.
Amesema Pakistan inapenda kushirikiana na China kuendeleza urafiki wa jadi, kuimarisha uratibu wa kimkakati wa mipango yao ya maendeleo, kupanua ushirikiano wa kivitendo, na kukuza kwa uthabiti ushirikiano wa hali zote wa kiwenzi na kimkakati kati ya China na Pakistan.
"Pakistan inasisitiza kushikilia kanuni ya kuwepo kwa China moja na itaendelea kuiunga mkono China bila kuyumbayumba katika masuala yote yanayohusu maslahi yake ya msingi," ameongeza Dar.
Pande zote mbili zimekubaliana kuimarisha mshikamano wa Nchi za Kusini ili kulinda maslahi ya pamoja, kushikilia Katiba ya Umoja wa Mataifa, na kupinga vitendo vya ukandamizaji ambavyo vinakiuka mamlaka ya nchi nyingine.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akiwa anafanya Duru ya Saba ya Mazungumzo ya Kimkakati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Pakistani na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistani Mohammad Ishaq Dar mjini Beijing, mji mkuu wa China, Januari 4, 2026. (Xinhua/Jin Liangkuai)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



