Rais wa Guinea ya Ikweta athibitisha mpango wa kuhamishwa kwa mji mkuu

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 05, 2026

YAOUNDE - Ofisi ya Kupashana Habari na Vyombo vya Habari ya serikali ya Guinea ya Ikweta imetangaza kuwa Rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang Nguema Mbasogo amethibitisha mpango wa kuhamishwa kwa mji mkuu wa nchi hiyo kutoka Malabo, ulioko Kisiwa cha Bioko, hadi mji wa bara wa Ciudad de la Paz katika Jimbo la Djibloho.

Ofisi hiyo imesema Obiang amesaini amri juu ya mpango huo wa kuhamishwa mji mkuu siku ya Ijumaa kwenye hafla ambayo maofisa wakuu wa serikali walishiriki.

Ciudad de la Paz, maana yake ni "Mji wa Amani," kuhamisha mji mkuu kuna madhumuni ya kuleta urahisi zaidi katika mawasiliano barabarani na kukabiliana na matatizo ya usafirishaji wa bidhaa na usalama yanayohusika na mji mkuu wa sasa wa Malabo ulioko kisiwani.

"Kwa mtazamo wa usalama, kuhamishwa kwa mji mkuu ni hatua muhimu, ikizingatiwa kwamba serikali imekuwa mwathirika wa mashambulizi kadhaa yaliyotoka nje ya nchi kwa kupitia njia za baharini," Ofisi ya Kupashana Habari na Vyombo vya Habari imesema katika taarifa yake.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kuhamishwa huko kwa mji mkuu pia kutawezesha nchi hiyo ya Afrika ya Kati kuvunja muundo wa zama za ukoloni uliopitwa na wakati, ambao hauchangii tena katika ujenzi wa mambo ya kisasa ya nchi hiyo.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kwamba itachukua muda wa mwaka mmoja kuhamisha huduma zote za mambo ya utawala hadi mji mkuu huo mpya.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha