China yalaani hatua za kijeshi za Marekani dhidi ya Venezuela kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 06, 2026

UMOJA WA MATAIFA - Sun Lei, Kaimu Balozi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa jana Jumatatu kwenye mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama uliofanyika kufuatia shambulio la Marekani dhidi ya Venezuela, amelaani vikali hatua za kijeshi za Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Amesema China imeshtushwa sana na inalaani vikali vitendo vya upande mmoja, visivyo halali, na vya ukandamizaji vinavyofanywa na Marekani.

"Januari 3, Marekani ilianzisha waziwazi mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya Venezuela, ikamkamata kwa nguvu Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na mkewe, na kuwasafirisha nje ya nchi. Ilidai kwamba 'itaiendesha' Venezuela na hata haikuondoa uwezekano wa kuanzisha raundi ya pili ya operesheni za kijeshi kwa kiwango kikubwa zaidi," amesema Sun.

Amesema kwa muda sasa, jumuiya ya kimataifa imekuwa ikieleza mara kwa mara wasiwasi mkubwa juu ya vikwazo, vizuizi, na vitisho vya kutumia nguvu vinavyotekelezwa na Marekani dhidi ya Venezuela. Hata hivyo, ikiwa nchi mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama, Marekani imepuuza wasiwasi huo mkubwa wa jumuiya ya kimataifa, ikikanyaga waziwazi mamlaka, usalama, pamoja na haki na maslahi halali ya Venezuela, na kukiuka kwa kiwango kikubwa kanuni za usawa wa mamlaka ya nchi, kutoingilia masuala ya ndani, utatuzi wa amani wa migogoro ya kimataifa, na marufuku ya matumizi ya nguvu katika uhusiano wa kimataifa.

Ameongeza kuwa China inatoa wito kwa Marekani kuhakikisha usalama wa Rais Maduro na mkewe na kuwaachilia mara moja.

"Masomo ya historia yanatoa onyo kali. Njia za kijeshi si suluhisho la matatizo, na matumizi holela ya nguvu yatasababisha tu migogoro mikubwa zaidi" amesema.

Amesema Marekani ililikwepa Baraza la Usalama ili kuanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya Iraq, ilishambulia waziwazi vituo vya nyuklia vya Iran, na kuweka vikwazo vya kiuchumi, mashambulizi ya kijeshi, na hata uvamizi wa kijeshi dhidi ya nchi nyingi za Latini Amerika na Karibiani. Vitendo hivi vimesababisha migogoro ya muda mrefu, ukosefu wa utulivu, na mateso makubwa kwa watu wa kawaida," amesema.

"China inapenda kushirikiana na nchi za kikanda na jumuiya ya kimataifa ili kuimarisha mshikamano na ushirikiano, kushikilia haki na usawa, na kulinda kwa pamoja amani na utulivu katika Latini Amerika na Karibiani," amesema.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha