Rais Trump afikiria njia za kuipata Greenland ikiwemo matumizi ya jeshi la Marekani

(CRI Online) Januari 07, 2026

Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt amesema katika taarifa aliyoitoa jana Jumanne kuwa, Rais wa Marekani Donald Trump na timu yake wanafikiria "njia mbalimbali" za kuipata Greenland ya Denmark, ikiwemo "kutumia jeshi la Marekani".

Amesema kwamba Rais Trump ameweka wazi kwamba kuipata Greenland ni kipaumbele cha usalama wa taifa wa Marekani, na ni muhimu ili kuwazuia mahasimu wa nchi hiyo katika eneo la Aktiki.

Mshauri wa Usalama wa Mambo ya Ndani wa Marekani Stephen Miller alisema mapema Jumatatu kwamba hakuna yeyote atakayepigana na Marekani kama itajaribu kuiteka Greenland, ambayo ni eneo linalojitawala la Denmark.

Wakati huo huo, viongozi wa nchi saba za Ulaya jana Jumanne walithibitisha tena kwamba Greenland "ni ya watu wake," wakisisitiza kwamba masuala yanayohusu Denmark na Greenland lazima yaamuliwe pekee na Denmark na Greenland.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha