Ukraine, Ufaransa, Uingereza zasaini azimio la nia ya kupeleka vikosi vya mataifa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 07, 2026

KIEV – Ukraine, Ufaransa na Uingereza siku ya Jumanne zilisaini azimio la nia ya kupeleka vikosi vya mataifa mbalimbali vya kuunga mkono ulinzi, ujenzi upya na uhimilivu wa kimkakati wa Ukraine baada ya makubaliano ya amani kufikiwa, shirika la habari la kitaifa la Ukraine, Ukrinform limeripoti.

Nyaraka hiyo imesainiwa huko Paris na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.

Utiaji saini huo umefuatia mkutano wa Muungano wa Waliotayari (Coalition of Willing), ambao ulileta pamoja viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya, vilevile mjumbe maalumu wa Ikulu ya Marekani Steve Witkoff na Jared Kushner, mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Baada ya mkutano huo, Rais Zelensky amesema tayari kuna uelewa wa kina wa mfumo wa hakikisho la usalama kwa Ukraine.

Kwa upande wake Starmer amesema azimio hilo linaunda msingi wa kisheria kwa operesheni za vikosi vya nchi washirika katika mipaka ya Ukraine kama makubaliano ya amani yakifikiwa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha