Lugha Nyingine
Touadera ashinda uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Picha hii iliyopigwa Desemba 14, 2025 ikimwonyesha Faustin-Archange Touadera akitoa hotuba mjini Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati. (Xinhua)
YAOUNDE - Matokeo ya awali yaliyotolewa na Mamlaka ya Uchaguzi ya Kitaifa (ANE) Jumatatu jioni yanaonesha kuwa rais aliye madarakani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin-Archange Touadera, ameshinda uchaguzi wa rais kwa kupata asilimia 76.15 ya kura zote zilizopigwa.
Touadera yuko mbele zaidi ya wagombea urais wengine, wakiwemo pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Anicet-Georges Dologuele, aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 14.66 ya kura, na Henri-Marie Dondra, Waziri Mkuu mwingine wa zamani, aliyepata asilimia 3.19 ya kura zilizopigwa.
Kutokana na matokeo hayo, Mkuu wa ANE Mathias Barthelemy Morouba amesema kwamba Touadera, mgombea wa Vuguvugu la United Hearts," amechaguliwa kwa matokeo ya awali" kuwa rais wa jamhuri.
"Wapiga kura takriban milioni 2.3 walijiandikisha, na idadi ya watu walioshiriki kwenye upigaji kura imefikia asilimia 52.42, " Morouba amesema wakati akitangaza matokeo hayo.
"Asante kwa watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kwa asilimia 76.15 ya kura zilizopatikana katika duru ya kwanza, kutokana na matokeo ya awali yaliyotangazwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchaguzi, azma yenu inastahili kupongezwa. Tutaendelea kufanya juhudi pamoja, " Touadera amesema kwenye majukwaa rasmi ya kampeni ya mitandao ya kijamii muda mfupi baada ya matokeo hayo kutangazwa.
Katika kampeni yake, Touadera, mwenye umri wa miaka 68, alisisitiza kurejesha amani na kuhimiza maendeleo katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita. Na amekuwa madarakani tangu mwaka 2016, katika uchaguzi huu akitafuta awamu yake ya tatu ya rais wa nchi hiyo.
Matokeo hayo ya awali yatawasilishwa kwa Mahakama ya Katiba ya Nchi, ambayo itasikiliza maombi ya walalamikaji kabla ya kuthibitisha matokeo ya mwisho ifikapo Januari 20.
Upigaji kura katika nchi hiyo ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, katika uchaguzi wa rais, wabunge, mikoa na manispaa ulifanyika Desemba 28, 2025.

Mathias Barthelemy Morouba, Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchaguzi, akisoma matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais, mjini Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Januari 5, 2026. (Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



