Vurugu zinazoongezeka zafanya watu makumi kwa maelfu kukimbia eneo la Kordofan la Sudan

(CRI Online) Januari 07, 2026

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric, amesema vitendo vya kikatili vinavyozidi kuongezeka nchini Sudan, hasa katika sehemu mbalimbali za eneo la Kordofan, vinaendelea kuwaweka raia katika hatari kubwa na kusababisha mawimbi mapya ya wakimbizi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumanne, msemaji huyo kwa kurejelea ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu amesema kati ya Oktoba 25 na Desemba 30, watu takriban 65,000 wamelazimikika kukimbia makazi yao kutoka maeneo mbalimbali ya Kordofan.

“Katika Jimbo la Kordofan Kusini, idadi ya wakimbizi imeongezeka ghafla kwa kiasi kikubwa katika siku za karibuni” amesema, akirejelea makadirio ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji kuwa kati ya Desemba 31 mwaka 2025 na Januari 4 mwaka huu, vurugu zilisababisha karibu watu 1,000 kukimbia eneo la Quoz, mji wa Kadugli na kijiji cha Berdab.

Amesema Jumatatu wiki hii watu wengine 2,000 walikimbia makazi yao kutoka eneo la Um Dam Haj Ahmed katika Jimbo la Kordofan Kaskazini.

Bw. Dujaric pia ameongeza kuwa mashirika ya kibinadamu yameripoti kutokea kwa shambulizi la droni katika mji wa El Obeid, linalodaiwa kusababisha vifo vya watu 13 wakiwemo watoto.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha