Lugha Nyingine
Kenya yajipanga kufufua tasnia ya korosho ili kukuza uchumi
Kenya inalenga kuzalisha nafasi za ajira takriban laki 3.5 na kuwekeza shilingi bilioni 30 za Kenya kupitia ufufuaji wa tasnia ya korosho inayosusua ya nchi hiyo.
Akizungumza na wakulima na wafanyakazi wa kuchakata korosho jana Alhamisi katika Kaunti ya Kilifi, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo nchini Kenya, Mutahi Kagwe, amesema miaka mingi ya kushuka mfululizo kwa uzalishaji kumeigharimu nchi hiyo ajira, mapato ya taifa na mapato ya mauzo ya nje, wakati mahitaji ya zao hilo duniani yakiendelea kuongezeka.
Kagwe amesema, mpango huo wa serikali unajikita katika sayansi na uungaji mkono wa wakulima, ukiongozwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo (KALRO), haswa kituo chake cha Mtwapa, ambacho kinajihusisha na utafiti wa korosho pekee.
Amesema Kituo hicho kimeendeleza aina mpya ya korosho ambayo ni himilivu kwa magonjwa na yenye uwezo wa kuongeza uzalishaji maradufu, huku miche elfu 20 ya aina hiyo iliyoboreshwa ikiwa tayari inapatikana kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima katika msimu ujao wa mvua.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



