Lugha Nyingine
Serikali ya Sudan yarudi Khartoum baada ya miaka karibu mitatu ya vita
Abdel Fattah Al-Burhan (kwenye gari), Mwenyekiti wa Kamati ya Mamlaka ya Mpito ya Sudan na Kamanda wa Vikosi vya Jeshi la Sudan (SAF), akiondoka kutoka Ikulu ya Rais mjini Khartoum, Sudan, Machi 26, 2025. (Picha na Tariq Mohamed/Xinhua)
KHARTOUM - Waziri Mkuu wa Sudan Kamil Idris ametangaza jana Jumapili serikali imerudi katika mji mkuu, Khartoum kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa vita Aprili 15, 2023, baada ya miaka karibu mitatu ya kuendesha mambo ya serikali katika mji wa mashariki wa Port Sudan.
"Serikali imerudi katika mji mkuu wa nchi," Idris amesema katika hotuba kwa umati wa watu baada ya kuwasili kwake Bahri, kaskazini mwa Khartoum.
Ameahidi kuboresha huduma za kimsingi, hasa katika sekta za afya na elimu, na kujenga upya hospitali na kurudisha ujenzi wa shule na vyuo vikuu, hasa Chuo Kikuu cha Khartoum.
Waziri Mkuu huyo ameongeza kuwa mwaka 2026 utakuwa "mwaka wa amani nchini Sudan," akizungumzia mipango ya ujenzi upya na maendeleo, vilevile juhudi za kuboresha hali ya uchumi kwa kupitia kuongeza pato la taifa, kupunguza mfumuko wa bei, na kutuliza kiwango cha kubadilisha fedha za nchi hiyo.
Kurudi huko kwa serikali ni sehemu ya juhudi rasmi za kurejesha kazi kuhusu mambo ya utawala na huduma za umma katika mji mkuu, kufuatia matangazo katika miezi ya hivi karibuni ya mipango ya hatua kwa hatua kurejesha taasisi za serikali, wakati huo hali ya usalama imekuwa nzuri katika baadhi ya maeneo, licha ya changamoto za usalama na ubinadamu zinazoendelea katika sehemu kadhaa za nchi hiyo.
Mji Mkuu Khartoum ulishuhudia mapigano makali yaliyosababisha uharibifu mkubwa kwa taasisi, miundombinu, na huduma za kimsingi za serikali.
Serikali ya Sudan ilihamia Port Sudan mwishoni mwa Aprili 2023, siku kadhaa baada ya mapigano kuzuka Khartoum kati ya Vikosi vya Jeshi la Sudan (SAF) na wanamgambo wa Vikosi vya Uungaji Mkono wa Haraka (RSF).
Mei 2025, SAF ilitangaza Jimbo la Khartoum kukombolewa kutoka kwa vikosi vya RSF, ikifungua njia kwa mji huo kumiliki tena maeneo ya umma hatua kwa hatua na kurejesha maisha ya kawaida.
Vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na mamilioni ya watu kupoteza nyumba za kuishi wakawa wakimbizi wa ndani ya Sudan au wa kuvuka mipaka yake.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



