Lugha Nyingine
Kanuni ya Kuwepo kwa China Moja ni msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya China na Afrika: Wizara ya Mambo ya Nje ya China
BEIJING - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning amesema jana Jumatatu kwamba kanuni ya kuwepo kwa China moja ni makubaliano ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa na kanuni ya msingi inayosimamia uhusiano wa kimataifa, pia ni msingi wa kisiasa wa uhusiano kati ya China na Afrika.
Mao Ning ameyasema hayo kwenye mkutano wa kawaida na waandishi wa habari alipoulizwa kutoa maoni kuhusu kauli za mamlaka za Taiwan juu ya kanuni ya kuwepo kwa China Moja, kama ilivyoelezwa kwenye taarifa ya pamoja ya Mazungumzo ya 9 ya Kimkakati kati ya China na Umoja wa Afrika (AU).
Amesema kwamba taarifa hiyo ya pamoja inaonyesha kikamilifu na kwa usahihi msimamo thabiti na usio na shaka wa upande wa Afrika kuhusu suala la Taiwan.
Amemnukuu Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf akisema katika mahojiano ya hivi karibuni kwamba "tutakuwa pamoja na China daima kuhusu suala la kanuni ya kuwepo kwa China Moja."
Mao ameeleza kuwa Mkutano wa Kilele wa Beijing wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) mwaka 2024 ulipitisha Azimio la Beijing.
"Nchi za Afrika zilizoshiriki na Kamisheni ya AU zilithibitisha tena uungaji mkono wao thabiti kwa kanuni ya kuwepo kwa China moja, zikisisitiza kwamba kuna China moja tu duniani, Taiwan ni sehemu isiyotengeka ya China, na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ni serikali pekee halali ya China, na ziliunga mkono juhudi za China za kufanikisha muungano wa kitaifa," Mao ameongeza.
"Tunazitaka mamlaka za Taiwan zikabiliane na hali halisi na kuacha michezo ya kisiasa ya kujidhalilisha na isiyo na uzito," Mao amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



