Lugha Nyingine
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Sri Lanka wakutana kuzungumzia uhusiano

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), akikutana na mwenzake wa Sri Lanka Vijitha Herath mjini Colombo, Sri Lanka, Januari 12, 2026. (Xinhua/Chen Dongshu)
COLOMBO - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi jana Jumatatu alifanya kituo cha mpito nchini Sri Lanka akiwa njiani kurudi kutoka ziara barani Afrika, na kufanya mkutano wa kirafiki na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sri Lanka Vijitha Herath. Amesema kwamba China iliipatia Sri Lanka msaada mapema iwezekanavyo kukabiliana na kimbunga kilichosababisha uharibifu mkubwa, na kwamba anaamini watu wa Sri Lanka wataweza kushinda janga hilo na kujenga upya makazi yao mapema.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amesema China inapenda kuimarisha ubadilishanaji wa uzoefu wa utawala na Sri Lanka, kupanua ushirikiano wa kivitendo katika nyanja mbalimbali, kuendeleza mawasiliano kati ya watu, kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiwenzi na kimkakati unaojengwa juu ya kusaidiana kwa dhati na urafiki wa kudumu kati ya nchi hizo mbili, na kujenga kwa pamoja jumuiya ya China na Sri Lanka yenye mustakabali wa pamoja.
Wang amesema kwamba katika mazingira ya kimataifa yanayozidi kuwa magumu na yasiyotabirika, China itadumisha kwa uthabiti kulinda haki na maslahi halali ya nchi zinazoendelea, hasa nchi ndogo na za kati, kushikilia madhumuni na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa, na kushirikiana na nchi zenye nia moja kupinga kurejea kwa "sheria ya mwituni," kukataa aina zote za siasa za umwamba na mabavu, na kulinda mfumo wa pande nyingi na haki na usawa wa kimataifa.
Wang ameeleza kuwa China inashukuru Sri Lanka kushikilia kanuni ya kuwepo kwa China moja kwa muda mrefu na inapenda kuendelea kuiunga mkono Sri Lanka katika kufuata njia ya maendeleo inayolingana na hali zake za kitaifa. Ameongeza kuwa pande zote mbili zinaweza kuimarisha ushirikiano wa kikanda unaolenga wa Asia Kusini na kwa pamoja kuhimiza ujenzi wa mfumo wa usimamizi wa duniani ulio wa haki na usawa zaidi.
Kwa upande wake Herath ameishukuru China kwa msaada wake muhimu kufuatia janga la kimbunga. Amesema Sri Lanka inaichukulia China kuwa mmoja wa washirika wake wa kimkakati wanaoaminika zaidi, na inapenda kudumisha mawasiliano ya karibu ya ngazi ya juu na China, kuimarisha ushirikiano katika miundombinu, masuala ya baharini, utalii, na mawasiliano ya kiutamaduni, na kuendelea kuinua kiwango cha ushirikiano wa kiwenzi na kimkakati kati ya Sri Lanka na China
Amesisitiza tena kuwa Sri Lanka itaendelea kufuata kanuni ya kuwepo kwa China moja, akaeleza uungaji mkono thabiti kwa juhudi za China za kulinda mamlaka na ukamilifu wa ardhi yake, na akasema Sri Lanka inapenda kuimarisha mawasiliano na uratibu na China katika mambo ya pande nyingi ili kulinda kwa pamoja haki na maslahi halali ya nchi zinazoendelea.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



