Lugha Nyingine
Kamishna wa EU asisitiza usalama wa Greenland, aonya kuwa hatua ya Marekani kuichukua itavunja NATO
Picha hii iliyopigwa Machi 19, 2025 ikionyesha mandhari ya Nuuk, mji mkuu wa Greenland, eneo linalojitawala la Denmark. (Xinhua/Zhao Dingzhe)
HELSINKI - Umoja wa Ulaya (EU) unaweza kutoa msaada wa kiusalama kwa Greenland endapo Denmark itaomba, Kamishna wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya ulinzi na anga ya juu Andrius Kubilius amesema, akionya kwamba hatua yoyote ya kijeshi wa Marekani dhidi ya eneo hilo la Aktiki itasababisha kusambaratika kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Akizungumza na vyombo vya habari jana Jumatatu pembezoni mwa mkutano wa usalama uliofanyika mjini Salen, Sweden, Kubilius amesema anaunga mkono kauli ya Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen kwamba hatua ya kulazimisha kuchukua eneo hilo itakuwa pigo kubwa kwa NATO na kuharibu vibaya uhusiano wa pande mbili za Atlantiki. Ameongeza kuwa hatua hiyo pia itasababisha mwitikio mbaya miongoni mwa nchi za Ulaya.
Rais wa Marekani Donald Trump akihudhuria mkutano na waandishi wa habari kufuatia mkutano wa viongozi wa NATO mjini The Hague, Uholanzi, Juni 25, 2025. (Xinhua/Zhao Dingzhe)
Kubilius amesema haamini uvamizi wa Marekani uko karibu, lakini amekumbusha kuwa Kifungu cha 42.7 cha mkataba wa EU kinazitaka nchi wanachama kutoa msaada wa pamoja endapo nchi mwanachama itakabiliwa na uvamizi wa kijeshi.
Amesema Umoja wa Ulaya unaweza kuongeza uungaji mkono kwa Greenland kwa ombi la Denmark, ikiwemo uwezekano wa kupeleka wanajeshi pamoja na kuimarisha miundombinu ya kijeshi, kama vile kuongeza uwepo wa vikosi vya majini na uwezo wa kukabiliana na droni.
Denmark na Marekani, zote nchi wanachama wa NATO, zimepanga kukutana wiki hii kujadili suala hilo la Greenland. Greenland na Denmark zimekuwa zikisema mara kwa mara kwamba eneo hilo haliuzwi, huku Rais wa Marekani Donald Trump akisisitiza kwamba Marekani lazima "iimiliki" Greenland bila kuondoa uwezekano wa kutumia nguvu.
Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson amesema nchi za Ulaya ndani ya NATO zilikuwa zikijadili njia za kuimarisha jumuiya hiyo, lakini amesisitiza kuwa juhudi hizo hazipaswi kujengwa juu ya dhana yoyote kwamba NATO inaweza kusitisha shughuli zake.
Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson akiwasili kwenye ukumbi wa mkutano maalum wa viongozi wa Umoja wa Ulaya (EU) mjini Brussels, Ubelgiji, Februari 1, 2024. (Xinhua/Zhao Dingzhe)
Pia kwenye mkutano wa sera za usalama mjini Salen, Kristersson juzi Jumapili alikosoa hatua za hivi karibuni za Marekani nchini Venezuela na "maneno ya vitisho" ya Trump kuhusu Denmark na Greenland, akionya kwamba hatua za namna hiyo zinadhoofisha sheria za kimataifa na kuongeza hatari kwa nchi ndogo.
Watu wakiandamana mbele ya Ubalozi wa Marekani mjini Copenhagen, mji mkuu wa Denmark, Machi 29, 2025. (Picha na Liu Zhichao/Xinhua).
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



