Lugha Nyingine
Watu 32 wauawa na wengine 86 kujeruhiwa katika mashambulizi ya droni ya RSF nchini Sudan
Angalau watu 32 wameuawa na wengine 86 kujeruhiwa katika mashambulizi ya droni katikati na kusini mwa Sudan yaliyofanywa na wanamgambo wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) jana Jumatatu, vyanzo vya habari nchini humo vimesema.
Chanzo cha habari ndani ya serikali katika Jimbo la Sinnar kimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba RSF imeua watu 27 na kujeruhi wengine 73 katika shambulizi la droni kwenye kambi ya kijeshi katika mji wa Sinja wa Jimbo la Sinnar katikati mwa Sudan, huku akiongeza kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka kutokana na hali mbaya ya majeruhi.
Shuhuda mmoja amesema shambulizi hilo lililenga makao makuu ya Divisheni ya 17 ya askari wa miguu ya Jeshi la Sudan na vituo vya kuzalisha umeme na maji vilivyo karibu.
Serikali ya Jimbo la Sinnar pia imetoa taarifa, ikisema Sinja ililengwa Jumatatu mchana kwa droni ya kimkakati ya RSF, na kwamba kikosi cha ulinzi wa anga cha jeshi la Sudan kilishambulia droni hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



