Vikosi vya Nigeria vyawaokoa abiria 18 wa Cameroon walioshambuliwa na washukiwa wa uharamia

(CRI Online) Januari 13, 2026

Jeshi la Nigeria limesema abiria wasiopungua 18 waliokuwa wakisafiri kwenda Cameroon wameokolewa na vikosi vya Nigeria baada ya kundi linaloshukiwa kuwa ni maharamia wa baharini kushambulia na kuteka boti ya abiria hao Jumatatu.

Mkurugenzi msaidizi wa uhusiano wa umma kwenye Makao Makuu ya Brigedi ya 13 ya Jeshi la Nigeria, Semi Sokoya, ameviambia vyombo vya habari huko Calabar, mji mkuu wa Jimbo la Cross River nchini Nigeria, kwamba tukio hilo lilitokea kwenye maji ya bahari kati ya Calabar na Cameroon, ambapo jeshi lilijibu mara moja baada ya kupokea simu ya dharura.

Sokoya amesema washukiwa hao wa uharamia walikuwa wakiendesha boti mbili za kasi na jahazi, ambapo walizuia boti hiyo ya kibiashara na kuwateka nyara abiria karibu na Kombo, bandari ya uvuvi iliyoko bahari ya Cameroon.

Amesema Jeshi la Nigeria lilichukua hatua mara moja na kuwasaka washukiwa hao, hatua iliyopelekea mapigano ya kufyatuliana risasi na kusababisha boti moja ya maharamia kupinduka. Sokoya amesema maharamia waliwaacha abiria na kukimbilia kwenye mto mdogo, na kwamba abiria wote wameokolewa bila kujeruhiwa.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha